SERIKALI YAIMARISHA RASILIMALI WATU SEKTA YA AFYA, KUKABILI MAGONJWA YA MLIPUKO
Posted on: June 6th, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Mafinga, Iringa
Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika sekta ya afya kama sehemu ya mkakati wa kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko nchini kupitia mafunzo mbalimbali yanayolenga kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika maeneo ya utayari, kinga na mwitikio wa haraka wakati wa dharura za afya ya umma.
Akifungua mafunzo ya utayari wa ugonjwa wa Ebola leo Juni 6, 2026 katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Bonaventura Chitopela, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa watumishi wa afya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na dharura nyingine za afya ya umma.
Amesema Serikali inaendelea kuweka kipaumbele katika kujenga uwezo wa wataalamu wa afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama, zenye ubora na zinazokidhi viwango vya kitaaluma wakati wote. Mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa kuhusu mbinu za utambuzi wa mapema, kinga, ufuatiliaji na mwitikio wa haraka endapo kutatokea tishio la ugonjwa wa Ebola.
“Uwekezaji katika mafunzo ya utayari wa Ebola unatuwezesha kuwa na mfumo imara wa kugundua mapema vihatarishi vya kiafya na kuchukua hatua stahiki kwa wakati, hivyo kulinda afya za wananchi wetu,” amesema Dkt. Chitopela.
Washiriki wa mafunzo hayo wamepatiwa elimu kuhusu dalili za ugonjwa wa Ebola, matumizi sahihi ya vifaa kinga binafsi, udhibiti wa maambukizi ndani ya vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na taratibu za kuripoti na kushughulikia wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo. Mafunzo hayo pia yamehusisha mazoezi kwa vitendo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mafunzo haya yanasaidia kuongeza umahiri wa wahudumu wa afya katika kufanya tathmini ya hatari, kuwasiliana kwa ufanisi wakati wa dharura na kutoa mwitikio wa haraka pale panapojitokeza tishio la ugonjwa wa mlipuko,” amesema Dkt. Chitopela.
Kwa upande wake, Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya, Bi. Theresia Haule, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuimarisha mfumo wa afya nchini kwa kuhakikisha watumishi wanakuwa na ujuzi na maarifa