SERIKALI YAIMARISHA ELIMU YA AFYA DHIDI YA EBOLA NCHINI
Posted on: May 31st, 2026Na Clement Robert, WAF – Dar es Salaam
Wizara ya Afya imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Ebola, huku ikisisitiza Tanzania bado ipo salama dhidi ya ugonjwa huo hatari
Akizungumza leo Mei 31, 2026 katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi msaidizi wa sehemu ya elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Rahma Hingora kutoka Wizara ya Afya amesema serikali inaendelea na kampeni maalumu ya kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ili kuongeza uelewa na kupunguza taharuki.
Dkt. Hingora amesema timu ya wataalamu wa afya imezunguka katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwakumbusha wananchi namna ya kujikinga pamoja na hatua za kuchukua endapo watabaini dalili zinazofanana na Ebola.
Amesema pamoja na kutoripotiwa kisa chochote cha ugonjwa huo nchini Tanzania, bado kuna umuhimu mkubwa wa wananchi kuwa makini kutokana na uwepo wa visa katika baadhi ya nchi jirani.
“kampeni hii inahusisha ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na wataalamu wa afya ngazi ya jamii, ambapo elimu inaendelea kutolewa katika vituo vya mabasi, masoko, shule na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu na kituo cha mabasi Magufuli ni miongoni mwa vipaumbele kutokana na kuwa kitovu kikubwa cha mabasi kutoka maeneo mbalimbali nchini” amesema Dkt. Hingora
Naye, Mkuu wa programu ya huduma za Afya ngazi ya jamii Dkt. Norman Jonas Kiara amesema wahudumu hao wamepewa jukumu la kutembelea nyumba kwa nyumba ili kutoa elimu ya kujikinga pamoja na kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa za dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa wa Ebola
“Moja ya changamoto kubwa ya ugonjwa wa Ebola ni kufanana kwa dalili zake na magonjwa mengine ya kawaida kama malaria, hali inayoweza kufanya wagonjwa kuchelewa kutambuliwa mapema kutokana na hali hiyo, serikali imeelekeza kuwa taarifa zote za watu wenye dalili zinazotia wasiwasi zichunguzwe mapema ili kubaini hali zao na kuchukua hatua stahiki kwa wakati