Wizara Ya Afya

SERIKALI YAFANIKIWA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI KANDA YA KASKAZINI

Posted on: October 8th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Tanga
 
Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa katika kikao kazi cha tathmini ya mwaka ya huduma za afya ya uzazi Kanda ya Kaskazini, zinaonesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vimeendelea kupungua kutoka vifo 168 mwaka 2021 hadi vifo 102 mwaka 2025 kati ya vizazi hai 100,000, huku msisitizo mkubwa ukitolewa juhudi zaidi kuendelea kufanyika ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi endapo kila mmoja katika nafasi yake atatimiza wajibu.
 
Hayo yameelezwa leo Oktoba 8, 2026, jijini Tanga na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya kina mama kutoka KCMC ambaye pia ni Kaimu mwenyekiti wa kanda Dkt. Bariki Mchome wakati akifungua kikao kazi cha tathmini ya mwaka ya huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa Kanda ya Kaskazini. Amewataka wasimamizi wa huduma katika ngazi ya halmashauri na mikoa kuhakikisha uwepo wa kanzi data za kufuatilia mama na mtoto na kuchukua hatua kwa wakati.
 
Dkt. Mchome ameeleza kuwa kupungua kwa vifo hivyo kumetokana na jitihada kubwa zinazofanywa na watumishi wa afya wanaohudumia wananchi usiku na mchana, sambamba na kipaumbele cha Serikali katika kuboresha afya ya uzazi na watoto wachanga.

Amesema katika kutekeleza azma hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, ameanzisha huduma za kambi za matibabu za Madaktari wa Mama Samia zinazozunguka nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo kwa vitendo watoa huduma katika kukabiliana na dharura za mama na mtoto.
 
Aidha, Dkt. Mchome amewataka washiriki wa kikao hicho kujadili kwa kina sababu zinazochangia vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga katika mikoa na halmashauri zao, ili kuandaa mikakati madhubuti ya kuhakikisha vifo hivyo vinaendelea kupungua na ikiwezekana kutokomea kabisa.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuweka mikakati ya kuboresha huduma kabla ya kujifungua, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, pamoja na kuboresha miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba katika vituo vinavyotoa huduma za mama na mtoto.