Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUPAMBANA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

Posted on: May 11th, 2026

Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza nchini kwa kuongeza huduma za matibabu, vifaa tiba pamoja na upanuzi wa huduma maalum katika hospitali mbalimbali nchini.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Mei 11, 2026 wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azan Zungu.

"Mzigo wa wagonjwa yasiyoambukiza umeongezeka kutoka wagonjwa milioni 6,502,913 mwaka 2024/2025 hadi kufikia wagonjwa milioni 6,874,308 Machi 2026, huku gharama za matibabu zikiongezeka kutoka Shilingi trilioni 1.3 mwaka 2023 hadi Shilingi trilioni 1.8 mwaka 2024," amesema Waziri Mchengerwa

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema Wizara ya Afya imeanzisha kliniki 130 za kisukari na shinikizo la damu na kufanya idadi ya kliniki hizo kufikia 168 nchini kote, huduma za dialysis zimeongezeka hadi kufikia kuwa na vituo 74 vinavyohudumia wagonjwa 3,342.

“Serikali imeendelea kuboresha huduma za magonjwa yasiyoambukiza ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na maeneo yao pamoja na kupunguza gharama za matibabu,” amesema Waziri Mchengerwa

Kwa upande wa afya ya akili, amesema huduma zimewafikia wateja laki 254,932 huku vituo 16 vya waraibu vikitoa huduma kwa wateja elfu 17,807 na upatikanaji wa dawa za afya ya akili kufikia wastani wa asilimia 75.

"Huduma za sikoseli zimeongezeka ambapo watoto 17,245 wamepimwa, watoto 369 kugundulika kuwa na ugonjwa huo na 2,500 kubainika kuwa na vinasaba vya sikoseli, wagonjwa 42,564 wamehudumiwa," amesema Waziri Mchengerwa

Katika huduma za kinywa na meno, Waziri Mchengerwa amesema Serikali imeongeza viti 26 vya huduma na kufikisha jumla ya viti 900 pamoja na kuongeza mashine za mionzi, pia huduma za macho katika mikoa 15 zimewanufaisha watu 51,940.