Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUKABILIANA NA MADUKA YA DAWA YASIYO NA VIBALI

Posted on: April 23rd, 2026

Na Shaban Juma, Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kudhibiti uwepo wa maduka ya dawa yasiyo na vibali, pamoja na vitendo vya utoaji wa dawa kiholela na uuzaji wa bidhaa zisizoruhusiwa.

Dkt. Samizi amesema hayo leo Aprili 23, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kaskazini, Mhe. Adonis Alfred Bitegeko, aliyetaka kujua lini changamoto hiyo itapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) pamoja na Baraza la Famasi inaendelea kusimamia na kufuatilia mwenendo wa utoaji wa huduma za dawa nchini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Ameeleza kuwa hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kusitisha huduma mara moja kwa watoa huduma wanaokiuka taratibu, pamoja na kuwaelekeza kufuata sheria na kanuni zilizowekwa, hususan kwa wanaotoa huduma bila vibali, wanaouza dawa zisizoruhusiwa na wasiokuwa na wataalamu wenye sifa za famasi.

Aidha, ametoa rai kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuendelea kuimarisha usimamizi kupitia timu za afya katika maeneo yao ili kuhakikisha maduka ya dawa yanaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya kitaifa.

Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa wote wanaokiuka taratibu ili kulinda afya na usalama wa wananchi.