SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI SEKTA YA DAWA NA VIFAA TIBA
Posted on: May 8th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam
Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya dawa, vifaa tiba na teknolojia za afya kwa lengo la kuongeza ushindani wa Tanzania katika uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, anaeshuhulikia Dawa na Vifaa Tiba Bw. Emmanuel Tayari amesema hayo leo Mei 08, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uendeshaji wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba katika eneo la Mloganzira Jijini Dar es Salaam.
"Maeneo haya ya Mloganzila na Kibaha yamepewa kipaumbele kutokana na ukaribu wake na taasisi kubwa za elimu, utafiti na huduma za afya, hali inayorahisisha upatikanaji wa wataalamu, teknolojia na maarifa muhimu kwa maendeleo ya sekta hii," amesema Bw. Tayari
Amesema Serikali imechagua kuanza na maeneo hayo mawili ili kujenga uzoefu wa utekelezaji, kuboresha mifumo ya kazi na kuandaa mfano utakaotumika katika maeneo mengine nchini ikiwemo Kilimanjaro, Mbeya na Mtwara.
Aidha, Bw. Tayari amesema Wizara ya Afya imepatiwa ekari 100 katika eneo la Bagamoyo kupitia 'Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority' (TISEZA) kwa ajili ya kuanzisha Bio-Industrial Park itakayosaidia kuvutia uwekezaji mkubwa katika viwanda vya dawa, chanjo na bidhaa nyingine za afya.
"Bagamoyo ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha muda mrefu cha viwanda vikubwa kutokana na ukubwa wa eneo na uwezekano wa kuanzisha miundombinu maalum kwa ajili ya wawekezaji wa sekta ya afya na teknolojia za kibaiolojia," amesema Bw. Tayari
Pia, amesema Serikali imeamua kutumia mfumo wa “cluster” ili kupunguza gharama za uwekezaji zinazotokana na miundombinu, nishati, maji, mifumo ya ubora, usalama pamoja na taratibu za usajili na vibali.
“Tunataka wawekezaji wanapokuja Tanzania wakute mfumo tayari umeandaliwa, wenye miundombinu, taasisi za udhibiti na mazingira rafiki ya utekelezaji wa miradi yao,” amesema Bw. Tayari.
Mwisho, ameishukuru TISEZA kwa ushirikiano wake katika kutenga eneo hilo, akisisitiza kuwa agenda ya maendeleo ya sekta ya dawa na vifaa tiba ni agenda ya Serikali nzima inayohitaji ushiriki