SERIKALI YADHAMIRIA KUIMARISHA HUDUMA ZA DHARURA NCHINI
Posted on: June 12th, 2025
Na WAF MOROGORO.
Serikali imeendelea kuiishi adhma yake ya kuokoa maisha na kulinda uhai wa wananchi kwa kuimarisha huduma za Dharura za kimatibabu kwa wagonjwa wa ndani na nje ya hospitali ili kuendana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya Sita.
Hayo yamebainishwa Juni 11, 2025 mkoani Morogoro na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Majanga Wizara ya Afya Dkt. Erasto Slyvanus kwamba Serikali katika kulifikia hilo inaendesha mafunzo yanayolenga kuimarisha huduma za dharura katika hospitali za halmashauri, mikoa kanda. na taifa.
Dkt. Sylvanus amesema walimu wateule kutoka mikoa 10 nchini watafundishwa na wakufunzi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili.
“Hawa tunaowafundisha wamechaguliwa kutoka mikoa 10 ya Tanzania bara kuwakilisha wengine, baada ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika kipindi hiki cha miaka minne, kwa kujenga idara za dharura na vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) kwenye ngazi zote mpaka ngazi za halmashauri na kuweka vifaa vya kutosha vya kisasa,” amesema Dkt. Sylvanus.
Amesema Serikali imeona kuna haja ya kuwafundisha wataalam wanaofanya kazi katika vituo hivyo ili wawe na weledi na ujuzi wa kutumia vifaa hivyo na kutoa huduma bora kuongeza tija inayoendana na thamani ya uwekezaji huo.
“Mafunzo haya sasa yanalenga kuwaimarisha katika namna bora ya kutoa huduma za dharura na walimu hawa wakishakamilisha mafunzo watarejea katika mikoa yao na kuwafundisha wenzao ili kusaidia mikoa kwenye kutoa na kuboresha huduma,” amesema Dkt. Sylvanus.
Aidha Dkt. Sylvanus amewakumbusha watoa huduma za dharura kuhakikisha wanalinda uhai kwanza pale inapotokea dharura yoyote ya kimatibabu ya nje na ndani ya hospitali na hata zile za usafiri wa dharura kisha uchangiaji wa huduma ufuate baadaye.