SERIKALI, WADAU WAWEKA MIKAKATI YA PAMOJA KUBORESHA SEKTA YA AFYA.
Posted on: May 26th, 2025
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais- TAMISEMI imefanya kikao maalum cha mashauriano ya kiufundi na wadau wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia, Shirika la GFF la Marekani, JICA kutoka Serikali ya watu wa Japan na KFW ya Ujerumani, ikiwa ni hatua za awali za maandalizi ya utekelezaji wa Mpango Endelevu wa Mageuzi na Ubunifu katika Sekta ya Afya (SHIFT).
Kikao hicho kilichofanyika kwa siku tano, Jijini Dar es Salaam na kuhitimishwa Mei 23, 2025, kililenga kubadilishana uzoefu wa kitaalam katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na mipango mahususi ya kuharakisha utekelezaji wa afua za uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya hapa nchini.
Akifungua rasmi kikao hicho, Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Bw. Amoury Amoury, amesisitiza dhamira ya kikao hicho maalumu katika kuweka misingi imara ya utekelezaji wa Mpango wa SHIFT kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa, ikiwa ni pamoja na: kuimarisha huduma za dharura na magonjwa ya mlipuko, utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI), kuboresha mifumo ya afya ya jamii na huduma za magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), miundombinu ya maabara, na mifumo ya kidijitali ya afya.
Katika kikao hicho, Serikali na wadau wa maendeleo wamejadili malengo mahsusi, maeneo ya matokeo makubwa, viashiria , mipango ya utekelezaji, na masuala ya ulinzi wa kijamii na kimazingira yanayohusiana na mikakati ya utekelezaji wa Mpango.
Aidha kupitia kikao hicho shirikishi, Serikali imebainisha dhamira yake ya kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya Afya inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo inaratibiwa kwa pamoja, ili kuchangia katika maeneo ya vipaumbele vya sekta ya afya kama vile Rasilimali Watu, Afya ya Mama na Mtoto, Takwimu, Ubora wa Huduma, na Usimamizi madhubuti.
Dkt. Moustafa Abdalla kutoka Benki ya Dunia, kwa niaba ya wadau wa maendeleo, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi ya ushirikiano katika utekelezaji wa afua mbalimbali katika sekta ya Afya hapa nchini.
Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais- TAMISEMI zimetoa pongezi za dhati kwa Benki ya Dunia ikishirikiana na GFF, JICA na KFW kwa kuendelea kuwa washirika wa karibu katika kutoa ushauri wa kitaalam na kifedha ili kuhakikisha kuwa huduma bora za afya zinawafikia Watanzania wote.