Wizara Ya Afya

SERIKALI , WADAU WA MAENDELEO KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO KULETA MAGEUZI SEKTA AFYA

Posted on: June 5th, 2026


Serikali na wadau wa maendeleo kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kuharakisha mageuzi ya sekta ya afya kupitia utaratibu wa kuandaa mipango mikakati, utekezaji, ufuatiliaji na tathmini kwa pamoja kupitia mifumo wa Sector Wide Approach(SWAp) ambapo Tanzania ni nchi mojawapo Afrika inayofanya vizuri kwa takribani miaka 26. Ushirikiano huu unasaidia uimarishaji wa mifumo ya utoaji huduma za Afya nchini.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Juni 5, 2026 wakati akifungua kikao cha wadau wa Maendeleo wa Sekta ya Afya kilichofanyika jijini Dar es Salaam chini ya kaulimbiu isemayo “Kuharakisha Mabadiliko ya Mfumo wa Afya kupitia Ufadhili Endelevu, Mifumo Imara na Ushirikiano wa Kimkakati.”

Dkt. Shekalaghe amesema kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni hatua muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote bila kuwa na mzigo wa kifedha hivyo mafanikio ya mageuzi hayo yatategemea uwepo wa mifumo ya afya madhubuti , usimamizi bora, rasilimali watu za kutosha, miundombinu imara pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma, sekta binafsi, taasisi za dini na wadau wa maendeleo.

“Tunatambua kuwa kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote kunahitaji uwekezaji wa muda mrefu, mifumo imara ya usimamizi na ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi wote kwa usawa,” amesema.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya ndani ya nchi, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza usalama wa afya wa taifa, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuendelea kuzalisha fursa za ajira kwa Watanzania.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zinaendana ya Agenda 2063 Afrika Tuitakayo ambayo inasisitiza kujitegemea kwa bara la Afrika kupitia uwekezaji katika sekta za kimkakati, ikiwemo afya.