SERIKALI KUKABILIANA NA MATUKIO YA DHARURA NA MAJANGA NDANI NA NJE YA NCHI
Posted on: June 4th, 2026Na Zakayo Mosha WAF-Morogoro
Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Dharura na Maafa inaendelea kutekeleza afua za Kuimarisha utayari na uwezo wa kukabiliana na Majanga na dharura zingine za afya ya jamii ikiwemo kutuma timu za haraka za kukabiliana na matukio ya Dharura hizo (Deployment of Rapid Response Team) kwa lengo la kukabiliana na matukio ya dharura ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa Leo tarehe 4 Juni, 2026 Mkoani Morogoro na Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Maafa Wizara ya Afya Dkt. Erasto Sylvanus wakati akifungua kikao kazi cha timu ya Wataalam kutoka Wizara mtambuka kwa dhana ya Afya moja kushiriki zoezi la "table-top simulations exercise" ili kupima kwa vitendo matumizi ya Mwongozo wa Kutuma Timu ya Wataalam kukabiliana na dharura ndani na nje ya nchi (Personnel Deployment Guideline).
Amesema kuwa, Tanzania kupitia Wizara ya Afya Kitengo cha Dharura na Maafa imeendelea kujiimarisha na kujipanga vema kwa kuwaandaa Wataalam wa Afya kuweza kukabiliana na Majanga na dharura zinazoweza kujitokeza kama vile Ebola, Marburg na dharura zingine zenye athari kwa Afya ya jamii.
"Napenda kuwahakikishia Wananchi na jamii ya Watanzania kuwa Serikali yetu imejizatiti kuchukua tahadhari katika maeneo yote ikiwemo mipakani mwa Nchi zilizokumbwa na ugonjwa wa Ebola kama Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na katika jamii kwa ujumla. Wataalam wa Afya wamejipanga na elimu mbalimbali inaendelea kutolewa kwa Wananchi ili waendelee kuchukua tahadhari ili ugonjwa usiingie nchini", amesema Dkt.Erasto Sylvanus
Aidha, Dkt.Erasto amewashukuru Wataalam wa Afya hapa nchini kwa jinsi wanavyoendeleea kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma bora kwa Wananchi wakati wa Dharura na Majanga na kuwataka wataalam hao kuwa tayari kuwasaidia wenzetu wa Nchi zingine zilizoathirika wakati huu wanapopita katika hatari ya ugonjwa wa Ebola kutokana na uwezo mkubwa wa wataalam wetu na mafunzo mbalimbali waliyopata.