SERIKALI KUIMARISHA MIFUMO YA MAABARA KUPITIA TATHMINI YA UKOMAVU WA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: May 15th, 2026
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Africa CDC imeendelea kuimarisha huduma za maabara nchini kwa kuandaa tathmini maalumu ya kupima ukomavu wa mifumo ya maabara, ikiwa ni hatua inayolenga kuimarisha huduma za afya, kuongeza ubora wa uchunguzi wa magonjwa pamoja na kuimarisha usalama wa afya kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi na Matengenezo ya Vifaa Tiba, Dkt. Alex Magesa wakati wa zoezi la kutathmini ukomavu wa mifumo ya huduma za maabara nchini lililofanyika Dar es Salaam.
Dkt. Magesa amesema tathmini hiyo ya kimataifa inayojulikana kama Ufuatiliaji wa Ukomavu wa Maabara inafanyika kwa ushirikiano wa wataalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya, taasisi za afya, wadau wa maendeleo pamoja na mashirika ya kimataifa yanayoshirikiana na Serikali katika sekta ya afya.
Dkt. Magesa amesema zoezi hilo linalenga kubaini kiwango cha uwezo wa mifumo ya maabara nchini katika utoaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa, usimamizi wa ubora wa huduma, usalama wa maabara pamoja na uwezo wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa na changamoto nyingine za kiafya.
“Serikali imeeleza kuwa matokeo ya tathmini hiyo yatasaidia kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha uwekezaji katika sekta ya maabara, kuboresha miundombinu, kuongeza idadi ya wataalamu pamoja na kuhakikisha huduma za uchunguzi zinatolewa kwa ubora unaokidhi viwango vya kimataifa,” Amesema Dkt. Magesa
Kwa upande wake, Mratibu wa Maabara kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Maria Kelly amesema kuwa utekelezaji wa zoezi hilo unafanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali, Shirika la Afya Duniani na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC).
Ameongeza kuwa wataalamu wa kimataifa kutoka Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa (Africa CDC) wameshirikiana na timu ya kitaifa kufanya tathmini katika maeneo mbalimbali ikiwemo usimamizi wa miundo ya kiutawala, ubora wa huduma, taarifa za afya, usalama wa viumbe hatarishi pamoja na matumizi sahihi ya vifaa tiba katika maabara.