Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA SARATANI NCHINI - DKT. BITEKO

Posted on: May 2nd, 2024



Na WAF - Dar Es Salaam

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za Saratani na vifaa tiba ili kutanua wigo wa huduma za Saratani nchini na hivyo kuwezesha upatikanaji wa huduma hizo kwa urahisi.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Mei 2, 2024 wakati akimwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa Kituo cha Matibabu ya Saratani cha Aga Khan, Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Dkt. Biteko amesema mradi huo wenye thamani ya jumla ya Euro milioni 13.3 (shilingi 35 bilioni) umekuwa na mafanikio mbalimbali ndani ya miaka minne ya utekelezaji wake ikiwemo kutoa mafunzo kwa wahudumu 464 na watumishi 400 ngazi ya jamii kuhusu huduma za saratani.

Kupitia mradi huo wanajamii zaidi ya milioni 4.5 wamepewa elimu kuhusu Saratani, watu takriban laki 700,000 wamepimwa Saratani na zaidi ya wagonjwa wapya 39,093 kugunduliwa kuwa na Saratani kupitia vipimo stahiki na hivyo kuwawezesha kuanza kupata tiba stahiki.

Pia ametoa agizo kwa kituo hicho cha Aga Khan kushirikiana na vituo vingine vya matibabu ya Saratani nchini hususan Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji madhubuti wa huduma za tiba za mionzi na hivyo kupunguza msongamano wa wagonjwa Ocean Road.

Awali, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu alisema kuwa changamoto ya saratani nchini ni kubwa ambapo kila mwaka kuna wagojwa wapya 40,000 huku vifo 27,000 na kwamba saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi kwa asilimia 23.5.

Amesema uboreshaji wa huduma za afya nchini unaendelea ili kutimiza dhima ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha utoaji wa huduma za kisasa za Afya kwa wananchi ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan, Mwana Mfalme Bi. Zahra Aga Khan amesema kujengwa kwa kituo hicho ni ushahidi wa namna Tanzania inavyopiga hatua kwenye Sekta ya Afya kwa kutumia pia teknolojia ya hali ya juu ya kisasa kwenye matibabu.