Wizara Ya Afya

SAMIZI: UBORA WA HUDUMA ZA AFYA UNAHITAJI WITO, MAADILI NA USIMAMIZI THABITI

Posted on: October 20th, 2026

Na Shabani Juma, WAF – Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha maadili, wito na uwajibikaji kwa watumishi wa afya ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta hiyo unaleta matokeo chanya kwa wananchi.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI jijini Dodoma, Oktoba 20, 2026, Dkt. Samizi amesema ubora wa huduma za afya unahitaji ushirikiano wa wadau wote, huku maoni na mrejesho wa wananchi ukitumika kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuzitatua.

Amesema pamoja na kuwepo kwa madaktari, vifaa tiba, dawa na miundombinu ya kutolea huduma, bado kuna umuhimu wa kuimarisha namna watumishi wanavyowahudumia wagonjwa, ikiwemo mawasiliano mazuri, kueleza taratibu za matibabu na kuwajibu wagonjwa kwa heshima.

Ameeleza kuwa huduma bora hazitegemei utaalamu pekee, bali pia zinahitaji watumishi wenye maadili, wanaowajibika na kutambua umuhimu wa kumhudumia kila mgonjwa kwa kuzingatia mahitaji yake.

Aidha, Dkt. Samizi amesisitiza umuhimu wa kusimamia vigezo vya udahili na mafunzo katika vyuo vinavyozalisha wataalamu wa afya ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaohitajika katika utoaji wa huduma. Amesema taaluma za afya zinahitaji mafunzo ya vitendo kwa kuwa wataalamu hao wanatarajiwa kushughulikia maisha na afya za wananchi.

Ameeleza kuwa kutokuzingatia vigezo vya mafunzo na taratibu za kitaaluma kunaweza kuhatarisha usalama wa wagonjwa, hivyo ni muhimu kuimarisha usimamizi wa taasisi za mafunzo na kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi unaokidhi viwango vinavyotakiwa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amegusia changamoto za utekelezaji wa sera za afya, hususan upatikanaji wa huduma zinazotolewa bila malipo kwa makundi maalumu, yakiwemo watoto, wajawazito na wazee.

Amesema utekelezaji wa sera hizo unahitaji kuzingatia upatikanaji wa rasilimali na fedha za kugharamia huduma hizo ili kuhakikisha vituo vya afya vina uwezo wa kutoa huduma kwa makundi yaliyokusudiwa bila kuathiri utoaji wa huduma nyingine.