Wizara Ya Afya

SAMBAZENI MWONGOZO WA HEDHI SALAMA NA ZANA ZAKE KATIKA MAENEO YENU

Posted on: March 23rd, 2026

Na Said Nyaoza, WAF - Mbeya

Mkuu wa Sehemu Ndogo ya Afya Mazingira kutoka Wizara ya Afya Bw. Anyitike Mwakitalima amewataka Maafisa Afya wa wilaya na mikoa sambamba na waratibu wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Shuleni kutoka mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe na Rukwa kuhakikisha wanasambaza mwongozo wa hedhi salama na zana zake ili wananchi waweze kuusoma na kuuzingatia.

Bw. Mwakitalima ameelekeza hayo leo Machi.23, 2023 katika kikao kazi cha mafunzo ya usambazaji 'Dissemination' wa mwongozo huo kanda ya nyanda za juu kusini yanayofanyika jijini Mbeya.

"Nitumie fursa hii kuwaomba wote mlioshiriki mafunzo haya mwende mkafanye jukumu la kusambaza zaidi mwongozo huu katika maeneo yenu ya kazi kwani tunae mlenga ni mtumiaji wa mwisho ambae ni msichana na mwanamke walio katika umri wa kuzaa," Amesema Bw. Mwakitalima.

Bw. Anyitike amesema kupitia mwongozo huo ni lazima wanufaika wa hedhi salama watengenezewe mazingira mazuri ya upatikanaji wa bidhaa za Hedhi Salama na miundombinu yake kwa ajili ya kutumia na kufanya utakasishaji

"Tunapo zungumzia hedhi salama ni kitu cha kila mmoja wetu kwani ni jukumu letu sote, sio jukumu la msichana pekee wala la mama pekee bali kila mmoja ana nafasi yake ya kuweza kusababisha wasichana wanapata huduma za hedhi salama," amesema Bw. Mwakitalima

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Joyce Sigara amesema mwongozo huo ni ukombozi sio tuu kwa watoto wa kike bali kwa jamii nzima kwani ukimuelimisha mtoto wa kike umeelimisha jamii kiujumla wake.

Nae mwakilishi kutoka UNICEF Bi. Regnihaldah Mpete ameipongeza wizara ya afya kwa kuendelea kusimamia kwa ufasaha hatua ya usambazaji wa mwongozo huo na kuhakikisha afua zote zinatekelezwa kwa kufuata muongozo huo.

"Niwaombe wote walio shiriki mafunzo haya tuwe mabalozi wazuri katika utekelezaji wa mwongozo huu kwani bila kushirikiana na sekta tofauti hatuwezi kufanikiwa kuwa na hedhi salama katika jamii," amesema Bi. Mpete