ROF. SUNGUYA AKAGUA HALI YA HUDUMA ZA AFYA JNIA, ASISITIZA MIFUMO KUSOMANA KURAHISISHA UTENDAJI
Posted on: October 6th, 2026Na Andrea Kadege, WAF–Dar es Salaam
Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, leo Oktoba 6, 2026 ametembelea na kukagua vituo vya ukaguzi wa afya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, kwa lengo la kutathmini hali ya utoaji wa huduma, hususan katika maeneo yanayohusika na ufuatiliaji wa afya za wasafiri na magonjwa ya mlipuko.
Katika ziara hiyo, Prof. Sunguya ameambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Dharura na Maafa, Dkt. Erasto Sylvanus, pamoja na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Kinga, Dkt. Amour Seleman.
Prof. Sunguya amekagua mifumo na utendaji wa vituo hivyo, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa na ufuatiliaji madhubuti wa wasafiri pamoja na utambuzi wa mapema wa dalili za magonjwa ya mlipuko, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi wa afya ya jamii na usalama wa nchi.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko, ikiwemo Ebola ambayo inaendelea kuwa tishio katika baadhi ya nchi jirani, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha utayari na mifumo ya ufuatiliaji katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege.
Aidha, Prof. Sunguya amesisitiza umuhimu wa mifumo ya TEHAMA ya afya na ile ya uwanja wa ndege kusomana ili kurahisisha upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa muhimu, kuongeza ufanisi wa watendaji na kuwezesha hatua za haraka pale inapobainika hatari ya kiafya.
Ameelekeza pia hatua za ukaguzi na uboreshaji wa mifumo hiyo kuendelea katika viwanja vingine vya ndege nchini, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Arusha na Songwe, ili kuhakikisha viwango vya ufuatiliaji na tahadhari vinaendelea kuimarishwa.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Afya za kuimarisha utayari, ufuatiliaji na mwitikio wa afya katika maeneo ya kuingilia na kutoka nchini, kwa lengo la kuzuia na kudhibiti kuenea kwa magonjwa ya mlipuko na kulinda afya za wananchi na wasafiri.