MWANAMKE MWENYE UMRI WA MIAKA 34 AONDOLEWA UVIMBE KILO 8.6 KWENYE KIZAZI
Posted on: June 12th, 2025
Madaktari Bingwa wa magonjwa ya Wanawake na Uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke jana Juni 10, 2025 walifanya upasuaji wa kuondoa uvimbe wenye uzito wa kilo 8.6 kwa mwanamke (34) ambaye jina lake limehifadhiwa aliodumu nao kwa zaidi ya miaka mitano.
Upasuaji huo wa kibingwa ulifanyika kwa saa 3 chini ya uangalizi wa Dkt. Joseph Kiani pamoja na Daktari Evance Polin wote wakiwa ni madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi wakisaidiana na wataalamu wengine wa dawa na usingizi wakiongozwa na Dkt. Eva Shanga
Akizungumzia upasuaji huo Daktari bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dkt. Evance Polin alisema uvimbe wa aina hizo husababishwa na sababu mbalimbali lakini akina mama walio hatarini zaidi ni wale ambao wapo katika umri wa kuzaa lakini pengine hawajaweza kubeba ujauzito kwa sababu mbalimbali.
Aidha amezitaja dalili za vimbe hizo kuwa ni pamoja na mwanamke kutokwa na damu nyingi sana ukeni katika kipindi cha hedhi tofauti na siku za kawaida, mzunguko wa hedhi kubadilika mara kwa mara, kupatwa na maumivu makali kupita kiasi wakati wa hedhi na tumbo kuongezeka ukubwa kuliko kawaida na wakati mwingine huonekana kama tumbo la mjamzito.
Dkt. Polin amehitimisha kwa kutoa ushauri wa kitaalam kwa wanawake juu ya namna ya kuepuka changamoto za vimbe katika kizazi ambapo amewataka akina mama wote wanaotarajia kubeba ujazito au wale ambao tayari wanaujauzito na wanakumbana na dalili alizozitaja kuhakikisha wanaonana na madaktari bingwa wa wanawake na uzazi mapema iwezekavyo ili kujua afya zao za uzazi na kufanyiwa uchunguzi wa mapema
Hali ya mgonjwa kwa sasa inaendelea vizuri akiwa bado chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi ili kuhakikisha hali yake inazidi kuimarika na hatimaye anaruhusiwa kuondoka hospitali
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke ina jumla ya madaktari bingwa nane (8) wa magonjwa ya wanawake na uzazi wanaoendelea kutoa huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu kwa akina mama kwenye masuala ya uzazi na changamoto nyingine ambapo kiliniki ya kibingwa ya magonjwa ya wanawake na uzazi katika hospitali ya Temeke ni kila siku za jumatatu, jumatano na Alhamisi.