MOROGORO YAFANYA TATHMINI MATUKIO YA HATARI ZA KIAFYA , KUIMARISHA UTAYARI KUKABILIANA NA MAJANGA
Posted on: June 10th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Morogoro
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ametoa wito kwa watumishi wa sekta ya Afya na sekta mtambuka kuja na mikakati ya namna bora ya kuikinga jamii ya Morogoro na maafa, majanga na Athari za kiafya zitakazojitokeza
Dkt. Mussa ameyasema hayo leo Juni 10, 2026 wakati akifungua kikao kazi cha tathimini ya matukio na athari za kiafya za mkoa wa Morogoro. Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha utayari, kinga na uwezo wa kukabiliana na majanga mbalimbali yanayoweza kuathiri maisha ya wananchi na maendeleo ya mkoa huo.
Dkt. Mussa ameeleza kuwa Morogoro ni mkoa wa kimkakati unaounganisha maeneo mbalimbali ya nchi kupitia njia kuu nne za usafiri, hali inayochochea shughuli za kijamii na kiuchumi, lakini pia mwingililiano huo unaongeza uwezekano wa kukumbwa na majanga mbalimbali.
Aidha, Dkt. Mussa ametaja baadhi ya majanga yanayoweza kuikumba Morogoro kuwa ni magonjwa ya milipuko kama kipindupindu, M-pox na surua, mafuriko, maporomoko ya ardhi, athari za mabadiliko ya tabianchi, ajali za barabarani, majanga ya moto, matukio ya kemikali kumwagika pamoja na migogoro ya rasilimali.
“Maandalizi ya tathmini ya matukio na athari za kiafya (Regional Risk Profile) yatawezesha mkoa kubaini hatari zilizopo, kutathmini athari zake kwa wananchi na kuweka vipaumbele sahihi katika mipango ya maendeleo, bajeti na usimamizi wa dharura kwa kuzingatia ushahidi na takwimu sahihi,” amesema Dkt. Mussa
Ameongeza kuwa, zoezi hilo linaendana na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha maandalizi kabla ya majanga kutokea, sambamba na utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi wa Maafa (NDMS) 2022–2027.
“ Nitoe wito kwa washiriki kutumia uzoefu na takwimu sahihi za maeneo yao ili kuhakikisha nyaraka zitakazotokana na kikao hicho zinakuwa zinatekelezeka na kusaidia kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao pamoja na kuimarisha maendeleo ya Mkoa wa Morogoro kwa ujumla,”