Wizara Ya Afya

MHE. MCHENGERWA AWATAKA WATANZANIA KUJIKITA KATIKA KAZI NA KUEPUKA UCHOCHEZI

Posted on: June 26th, 2026

Na Clement Robert, WAF – Dodoma

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka Watanzania kuelekeza nguvu zao katika kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kujikita katika shughuli zenye tija kwa maendeleo ya taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuepuka vitendo vya uchochezi vinavyoweza kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuathiri kasi ya maendeleo ya nchi.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo, Juni 26, 2026, katika mahojiano na TBC baada ya kuahirishwa kwa Kikao cha 58 cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 13, kilichofanyika Bungeni, jijini Dodoma.

Amesema, msingi wa maendeleo ya kweli unategemea wananchi kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na shughuli za kiuchumi badala ya kujihusisha na mambo yanayoweza kusababisha migawanyiko ya kijamii au kuleta taharuki isiyo ya lazima, akibainisha kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo endelevu.

“Tukielekeza nguvu zetu kwenye kusimamia maendeleo ya nchi tutafanya mambo makubwa kwa ushirkiano na viongozi wetu kwenye serikali hii ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kila anapofanya maamuzi anafanya kwa mustakabali na maendelo ya wananchi wa taifa hili”

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kukuza sekta mbalimbali za kiuchumi, hususan sekta ya afya na viwanda, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja na maendeleo ya nchi yao.

Ameeleza kuwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika ujenzi na uboreshaji wa viwanda vya kuzalisha dawa nchini umeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa ndani wa kuzalisha dawa na vifaa tiba, hatua inayochangia kupunguza changamoto ya upungufu wa bidhaa hizo katika hospitali na vituo vya afya nchini.

Amesema kuongezeka kwa uzalishaji wa dawa ndani ya nchi kunapunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, jambo linalosaidia kuimarisha usalama wa afya ya wananchi, kupunguza gharama za uagizaji wa dawa kutoka nje na kuongeza ufanisi wa mfumo wa afya kwa ujumla.