Wizara Ya Afya

MCHENGERWA:BAJETI YALENGA KUIMARISHA UZALISHAJI BIDHAA ZA AFYA NDANI YA NCHI

Posted on: May 11th, 2026

Na Zakayo Mosha-WAF-Dodoma

Waziri wa Afya Mhe.Mohamed Mchengerwa ameliambia Bunge kuwa bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27 imepanga kujenga Viwanda vya ndani vya Uzalishaji wa bidhaa za Afya,lengo likiwa ni kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi am ambao umekuwa ukihitaji fedha nyingi kutoka Serikalini na kupunguza uwezo wa Serikali katika kutoa huduma nyingine kwa Wananchi.

Mchengerwa ameyasema hayo Mei 11,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwakilisha makadirio ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Sita Chini ya uongozi shupavu wa Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan umedhamiria kufanya Uwekezaji mkubwa wa kujenga Viwanda vya ndani vya bidhaa za Dawa

"Kufuatia agizo Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuimarisha uwezo wa nchi katika kuzalisha bidhaa za afya ili kufikia azma ya kujitosheleza kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2030, Wizara itaendelea kukiwezesha kikosi kazi maalum kuharakisha uwekezaji wa viwanda vipya vya bidhaa za afya nchini" amesema Waziri Mchengerwa

Aidha,ameliambia Bunge kuwa, Wizara ya Afya itaendelea kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuwawekea mazingira rafiki na wezeshi, ili kuwavutia kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya bidhaa za afya Kwa lengo la kupunguza utegemezi kutoka nje.

Aidha,amesisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga na imeshaelekeza Bohari ya Dawa Tanzania(MSD) kuhakikisha inanunua kwanza dawa zinazozalishwa ndani zilizokidhi vigezo vya TMDA kabla ya kwenda kununua nje ya nchi.ameongeza kuwa,Serikali imeamua kuchukua hatua za ukweli na uwazi ili kuhamasisha na kulinda uzalishaji wa dawa nchini.

Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa wawekezaji wa Ndani na nje ya nchi kuwezekeza katika Viwanda vya bidhaa za Dawa hapa Nchini ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje.amesisisitiza kuwa Dawa ni Tiba,Dawa ni uchumi ,Dawa ni Ulinzi na usalama wa Wananchi na Taifa kwa ujumla.