Wizara Ya Afya

MCHENGERWA: TMDA IVUTIE WAWEKEZAJI KATIKA UZALISHAJI WA DAWA NCHINI

Posted on: October 19th, 2026

Na. Andrew Kadege, WAF - Dodoma


Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuimarisha udhibiti wa dawa huku ikiweka mazingira wezeshi ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ili kuongeza uzalishaji wa dawa nchini.


Akizungumza Oktoba 19, 2026, jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Afya kwa TMDA, Mchengerwa amesema mamlaka hiyo ina nafasi muhimu katika kufanikisha azma ya Serikali ya kujitegemea kwa uzalishaji wa dawa.


“agenda yetu iwe udhibiti wa dawa, ushawishi wa wawekezaji wa ndani na nje, na ifikapo mwaka 2030 Taifa liwe na uwezo wa kuzalisha dawa zetu wenyewe,” amesema Mchengerwa.


Vilevile Mhe.Mchengerwa amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuzalisha nchini asilimia 80 ya mahitaji ya dawa na bidhaa za afya ifikapo mwaka 2030, hatua inayohitaji usajili wa bidhaa kwa wakati na ukaguzi wa viwanda kwa weledi bila kuathiri viwango vya ubora na usalama.


Ameongeza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo utasaidia kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na mapato ya Serikali, pamoja na kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi.


Aidha, ameitaka Bodi ya Ushauri kuhakikisha TMDA inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na uadilifu ili kulinda afya za wananchi na kuchochea maendeleo ya viwanda vya dawa nchini.