MCHENGERWA: DAWA BANDIA NI UHALIFU DHIDI YA WANANCHI
Posted on: October 19th, 2026Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb), ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuimarisha udhibiti wa dawa bandia na bidhaa za afya zisizokidhi viwango, akisema bidhaa hizo zinahatarisha maisha ya wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa TMDA, uliofanyika jijini Dodoma Oktoba 19, 2026, Mhe. Mchengerwa amesema udhibiti madhubuti unahitaji ujasiri, weledi na uadilifu, huku usalama wa wagonjwa ukipewa kipaumbele katika kila uamuzi. Amesisitiza kuwa TMDA inapaswa kukataa bidhaa au maombi ya usajili yasiyothibitisha usalama na ubora kwa mujibu wa ushahidi wa kisayansi, bila kujali ushawishi wa wawekezaji.
“Mdhibiti anayeogopa si mdhibiti; ni mhuri,” amesisitiza, akieleza umuhimu wa mamlaka hiyo kufanya maamuzi huru yanayolinda maslahi ya umma.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, ameitaka Bodi kusimamia uimarishaji wa ukaguzi wa bidhaa za afya sokoni na matumizi ya teknolojia kufuatilia bidhaa hizo kutoka kiwandani hadi kwa mtumiaji. Pia, amesisitiza ushirikiano kati ya TMDA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jeshi la Polisi, Mamlaka za Bandari, Uhamiaji na Serikali za Mitaa katika kudhibiti uingizaji na usambazaji wa bidhaa zisizo salama.
Vilevile, Waziri ameelekeza kuimarishwa kwa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kati ya TMDA na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ili mifumo ya bima izingatie usajili wa bidhaa za afya unaofanywa na TMDA.
Amesema hatua hizo zitasaidia kudhibiti bidhaa zisizo salama, kulinda maisha ya wananchi na kuimarisha imani ya umma katika mifumo ya udhibiti na utoaji wa huduma za afya nchini.