MAWENI HOSPITALI YAFANYA UPASUAJI WA NYONGA KWA MARA YA KWANZA
Posted on: May 31st, 2025
Na Mwandishi Wetu Kigoma
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji kwa mgonjwa mwenye tatizo la nyonga ikiwa ni siku ya tano ya kambi ya matibabu ya kibingwa na Ubingwa Bobezi katika hospitali hiyo.
Akizungumza na vyombo vya Habari Mei 30, 2025 mkoani Kigoma, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Joseph Nangawe amesema wananchi hawana budi kufika kupata huduma hiyo kwasababu wataalam wako makini pia mgonjwa uhudumiwa kwa umakini kuhakikisha anapata huduma bora.
“Hospitali na timu nzima ya upasuaji imefanya mandalizi ya kutosha kuanzia kuingia hospitali, hivyo niwahakikishie wananchi kuwa huduma hii ni salama lakini pia ni endelevu na leo ni upasuaji wa kwanza katika hospitali yetu,” amesema Dkt. Nangawe.
Pia Dkt. Nangawe amesema kuwa jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa kuwapeleka madaktri Bingwa na Bobezi katika hospitali za kanda pamoja na hospitali za rufaa ambao wanasaidia kutoa huduma kwa wananchi.
“Hizi ni jitihada za Serikali yetu ya awamu ya sita ambayo imekuwa ikileta madakitari Bingwa na Bobezi katika hospitali zetu za rufaa na ndiyo kinacho fanyika hapa leo,” amesema Dkt. Nangawe.
Hata hivyo Dkt. Wilson Masanja ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mifupa kutoka Hospitali ya Kanda Bugando Mwanza amesema, katika kambi hii ya siku tano huduma ya kumbadilishia nyonga mgonjwa ambaye amesumbuka kwa muda mrefu imefanyika huku akitoa wito kwa wananchi kutumia hospitali ya Maweni kupata huduma hizo kwani kuzifuata mbali ni gharama kubwa.
“katika huduma hii tuna asilimia 100 za upasuaji kwa sababu kila kilichotakiwa kufanyika kimefanyika na lengo ni kumfanya mgonjwa huyu atembee hivyo kwa matibabu haya mgonjwa atarudi katika hali yake ya kawaida,” amesema Dkt. Masanja.