MAPAMBANO DHIDI YA MALARIA, KIFUA KIKUU NA UKIMWI KUENDELEA KUTEKELEZWA HAPA NCHINI
Posted on: April 1st, 2026Na Atley Kuni, WAF-Dodoma
Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kujitegemea katika kugharamia na kutekeleza miradi ya afya, hususan ya kudhibiti Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI, katika kipindi ambacho misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali wa kimataifa inaendelea kupungua.
Akifungua kikao kazi cha siku mbili Aprili Mosi, 2026, jijini Dodoma,kikao kinachowakutanisha wadau wa Global Fund ,Dkt.Lazaro Hinga Meneja mradi wa Wizara ya Afya, amesema kuwa, sasa ni wakati wa Tanzania kusimama imara na kuendesha programu zake za afya kwa kutegemea zaidi rasilimali za ndani.
Amesema kuwa, kupungua kwa ruzuku kutoka kwa washirika wa maendeleo, hasa kufuatia mabadiliko ya sera katika nchi kama Marekani, kumezifanya nchi nyingi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, kukabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya sekta ya afya.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, Malaria bado ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa wagonjwa wanaofika vituo vya afya kwa karibu asilimia 30, huku Kifua Kikuu kikiathiri zaidi ya watu 130,000 kila mwaka na mara nyingi kuambatana na maambukizi ya UKIMWI.
"Kwa hivi sasa takwimu zinaonesha kuwa karibu watu milioni 1.7 hapa nchini wanaishi na virusi vya UKIMWI, licha ya mafanikio ya kupunguza maambukizi mapya" amesema Dkt. Hinga.
Dkt. Hinga amesema pengo la kifedha linaendelea kuwa kubwa, likifikia karibu asilimia 99 ya mahitaji katika baadhi ya programu, hali inayosisitiza umuhimu wa kujitegemea ili kulinda mafanikio yaliyopatikana na kuendelea kusonga mbele.
Amesema, kujitegemea kunatoa nafasi kwa nchi kupanga vipaumbele vyake kulingana na mahitaji halisi ya wananchi, kuimarisha uwajibikaji wa ndani, na kuhakikisha uendelevu wa huduma hata pale misaada ya nje inapopungua au kusitishwa.
Dkt. Hinga ameongeza kwamba, utegemezi wa muda mrefu kwa wahisani si suluhisho la kudumu katika sekta nyeti na muhimu kama afya.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali inaendelea kutekeleza mipango ya kuimarisha sekta ya afya, ikiwemo mpango wa Bima ya Afya kwa wote, unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wengi zaidi, kupunguza gharama za matibabu kwa mtu mmoja mmoja, na kuongeza vyanzo vya uhakika vya fedha za kuendesha miradi ya afya.
Sambamba na juhudi hizo za kifedha, Serikali imeweka mkazo zaidi katika mikakati ya kuzuia magonjwa kupitia hatua za kinga, ikiwemo kuhamasisha matumizi sahihi ya vyandarua vyenye viuatilifu ili kudhibiti Malaria, kuboresha mazingira ya makazi na usafi wa mazingira, ili kupunguza mazalia ya mbu, kuimarisha uchunguzi na matibabu ya mapema ya Kifua Kikuu, pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu njia za kujikinga na maambukizi ya UKIMWI.
Aidha, juhudi zinaelekezwa katika kuimarisha huduma za afya ngazi ya msingi, kuongeza upatikanaji wa chanjo na vipimo, pamoja na kuhimiza wananchi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kugundua magonjwa mapema. Elimu ya afya kwa umma imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kubadili tabia na kuongeza kinga dhidi ya magonjwa hayo.
Kikao hicho, kinatarajiwa kuweka mikakati madhubuti ya matumizi bora ya rasilimali chache zilizopo, huku kikionesha wazi kuwa Tanzania ipo tayari kujiimarisha kiuchumi na kuboresha huduma za Afya kwa Wananchi, kuhakikisha mapambano dhidi ya Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI yanaendelea kwa ufanisi bila kutegemea kwa kiasi kikubwa misaada kutoka nje ya nchi.