Wizara Ya Afya

Mageuzi ya Kidijitali Katika Sekta ya Afya Tanzania Yashika Kasi

Posted on: May 19th, 2026

Na John Mapepele
Geneva – Uswisi

Wakati dunia ikiendelea kuharakisha matumizi ya mifumo ya afya inayotegemea teknolojia ya kidijitali, Tanzania inaendelea kujijengea nafasi kama moja ya nchi zinazoongoza barani Afrika katika ujumuishaji wa teknolojia za afya.

Akizungumza katika mkutano pembeni mwa Mkutano Mkuu wa Afya Duniani (World Health Assembly) mjini Geneva, chini ya kaulimbiu “Kujenga Mifumo ya Afya ya Baadaye kwa Usawa na Upatikanaji katika Enzi ya Kidijitali: Kutoka Dira hadi Utekelezaji,” Mohamed Mchengerwa alieleza safari ya Tanzania katika kujenga mfumo wa afya ulio sawa, unaofikika kwa wote na wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto kupitia ubunifu wa kidijitali.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, ajenda ya afya ya kidijitali nchini Tanzania siyo tu kuhusu matumizi ya teknolojia, bali ni kuhusu kubadilisha maisha ya wananchi na kuhakikisha kila Mtanzania, bila kujali kipato chake au eneo analoishi, anapata huduma bora za afya.

“Kwa Tanzania, afya ya kidijitali siyo tu teknolojia. Ni kuhusu watu,” alisisitiza.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Tanzania imeandaa mikakati mbalimbali ya afya ya kidijitali yenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya. Hata hivyo, Waziri huyo alisema changamoto kubwa kwa sasa siyo tena kuwa na dira, bali ni utekelezaji wake.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imeamua kuondokana na miradi midogo midogo ya majaribio isiyounganishwa na kuelekea katika mifumo ya kitaifa inayoratibiwa na yenye uwezo wa kupanuka nchi nzima.

Mhe. Mchengerwa alieleza kuwa hapo awali Tanzania ilikuwa na mifumo mingi ya kidijitali ambayo haikuweza kuwasiliana yenyewe kwa yenyewe, jambo lililopunguza ufanisi katika sekta ya afya. Hata hivyo, hali hiyo ilibadilika chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan ambaye Serikali yake ilitoa msukumo mkubwa katika kuhakikisha mifumo hiyo inaunganishwa kitaifa.

Kwa sasa, Tanzania imeunganisha zaidi ya mifumo 45 ya afya ya kidijitali kupitia mfumo wa kitaifa wa mawasiliano ya mifumo hiyo (interoperability platform), hatua ambayo imewezesha takribani vituo 220 vya afya kuwasiliana kidijitali.