MAFUNZO YA WAKUFUNZI YALENGA KUIMARISHA UFANISI KWA AJIRA MPYA
Posted on: March 26th, 2026Na Happiness Hans, WAF- Morogoro
Mafunzo ya Wakufunzi (Training of Trainers – TOT) kwa Maafisa Rasilimali Watu, Tawala na Makatibu wa Afya yameelezwa kuwa nyenzo muhimu ya kuboresha utendaji kazi wa waajiriwa wapya serikalini.
Akizungumza Machi 25, 2026 kwa niaba ya Katibu Mkuu, Dkt. Seif Shekalange, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Bw. Issa N’gimba, amesema mafunzo hayo yaliyoidhinishwa na Wizara ya Afya yanalenga kuwajengea uwezo watumishi wapya ili wawe waadilifu, wawajibikaji na wenye ufanisi wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Amebainisha kuwa mafunzo hayo si tukio la mara moja, bali yanapaswa kuwa endelevu ili kuongeza ujuzi, kuimarisha utendaji na kupima mafanikio ya kazi, huku akisisitiza kuwa nafasi walizonazo washiriki ni muhimu katika kuathiri mwelekeo wa utendaji kwa watumishi wapya.
Bw. N’gimba ameongeza kuwa waajiriwa wapya hujifunza kwa kuangalia mienendo ya watumishi waliowakuta, hivyo ni wajibu wa washiriki kuwa mfano bora kwa vitendo.
Amewahimiza kuzingatia nidhamu kazini, ikiwemo mavazi yanayostahili, kuwahi kazini na kutekeleza majukumu kwa weledi na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Utumishi wa Umma kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, Bi. Verediana Ngahega, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia utu katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Amesema watumishi wa umma wanapaswa kuwasikiliza wananchi kwa heshima, staha na kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa Kitanzania.
Ameeleza kuwa kuzingatia utu katika utoaji wa huduma kutasaidia kupunguza malalamiko, kuimarisha mahusiano kati ya watumishi na wananchi, na hatimaye kuboresha mazingira ya kazi pamoja na ubora wa huduma zinazotolewa.