Wizara Ya Afya

MAFANIKIO YA UWEKEZAJI WA VIWANDA VYA DAWA NA VIFAA TIBA YANAHITAJI USHIRIKIANO

Posted on: May 8th, 2026


Mafanikio ya uwekezaji katika viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, wataalamu pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kurahisha upatikanaji wa bidhaa hizo nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amesema hayo leo Mei 08, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uendeshaji wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba katika eneo la Mloganzira Jijini Dar es Salaam.

"Matokeo yanayoonekana sasa katika sekta ya afya ni matunda ya kazi kubwa iliyofanywa na 'Pharmaceutical Industrial Acceleration and Facilitation Taskforce' (PIAT), kamati iliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kuharakisha uwekezaji katika sekta ya afya," amesema Dkt. Shekalaghe

Amesema kupitia kamati hiyo, Serikali imefanikiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha maamuzi yanafanyika kwa haraka na miradi ya uwekezaji inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amewapongeza viongozi na wataalamu wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weredi na kujituma kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya afya nchini.

Pia, Dkt. Shekalaghe amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo ya kazi na kuondoa changamoto zinazoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji katika sekta ya dawa na vifaa tiba.

"Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba kwa ajili ya soko la ndani na nchi nyingine za Afrika," amesema Dkt. Shekalaghe

Mwisho, amewahimiza watumishi wa sekta ya afya kuendelea kutoa huduma kwa weledi, huruma na uzalendo huku wakitambua kuwa mchango wao ni muhimu katika kufanikisha mageuzi ya sekta ya afya nchini.