Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA SAMIA 63 WAWEKA KAMBI MKOANI MWANZA

Posted on: June 16th, 2025

Na WAF, Mwanza


 Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wapatao 63 chini ya kampeni ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia  wameweka kambi kwa siku sita (6) mkoani Mwanza kwa ajili ya kutoa huduma za afya mkoani humo.


Akizungumza wakati wa mapokezi  ya madaktari hao leo Juni 16, 2025 Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza  Bw. Bw.Balandya Elikana  amesema, ujio wa madaktari hao ni neema kwakuwa afya bora huimarisha mwili na kuwa wenye nguvu na kufanya uzalishaji kwa mustakabali wa kuinua uchumi wa nchi.


Amesema, pamoja na mkoa huo kuwa na vituo vya kutolea huduma za afya 559 bado wanahitajika mabingwa kwa ajili ya huduma za kibingwa.


"Afya bora hupunguza mzigo kwa Wizara ya Afya, hivyo tunaipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza rasilimali nyingi zinazowezesha wananchi kupata huduma za afya hususan hizi zinazoshuka kwenye ngazi ya msingi," amefafanua  Bw. Elikana.


Katibu Tawala Bw.Elikana ametumia wasaa huo kuwaasa wananchi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwenye hospitali zote za wilaya pamoja na kisiwani Bwisya kupata huduma za afya kwa kufanya uchunguzi lakini pia kuwapatia elimu ya afya ya mwili.


Akizungumzia zoezi hilo Mwakilishi wa Wizara ya Afya Bi. Upendo Mamchony amesema Wizara inamshukuru Mhe. Rais kwa kampeni hii chanya ambayo wananchi wameipokea na kuipongeza.


"Mkoa wa Mwanza  watoa huduma 204 walijengewa uwezo katika awamu iliyopita, aidha watu zaidi ya 3000 walifikiwa na huduma kwa gharama ya chini na kwamba kwa sasa wanatarajia kuwafikia zaidi ya wananchi 4,000.


Naye Mganga Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba amesema madhumuni ya kampeni hiyo ni pamoja na kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi kwa kuwafuata wananchi walipo na wamedhamiria kuwahudumia wananchi wengi kwa gharama ndogo.


"Pamoja na hilo tunawategemea sana wataalam wetu wabobezi na mabingwa mlio kwenye kampeni hii, nawaomba mkawajengee uwezo wataalam mtakaowakuta kule na mkipata changamoto muda wowote msisite kuwasiliana nasi," amebainisha Dkt. Lebba.