MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAWAPIGA MSASA WATAALAM HOSPITALI YA GAIRO
Posted on: June 13th, 2025
Na WAF - GAIRO.
Wahudumu, Wataalam wa Afya hospitali ya wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuandaa mgonjwa kabla ya upasuaji, kuandaa chumba cha upasuaji na vifaa vya upasuaji kabla ya upasuaji, namna ya kufanya upasuaji salama na jinsi ya kufuatilia mwenendo wa wagonjwa baada ya upasuaji na timu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia.
Hayo yamebainishwa Juni 13, 2025 na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dkt. Chuma Novacatus wakati wa zoezi la Madaktari Bingwa wa Rais Samia linaloendele mkoani Morogoro katika halmashauri zote ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Gairo.
“Tumefanya mafunzo ya kuwezesha watumishi wa hospitali ya wilaya ya Gairo, namna ya kuandaa mgonjwa kabla ya upasuaji, kuandaa chumba Cha upasuaji na vifaa vya upasuaji kabla ya upasuaji, na namna ya kufanya upasuaji salama na jinsi ya kufuatilia mwenendo wa wagonjwa baada ya upasuaji,” amesema Dkt. Novacatus.
Dkt. Novacatus amesema mafunzo hayo yalianza kwa nadharia kisha kufanyika kwa vitendo ndani ya chumba cha upasuaji wakati upasuaji ukiendelea.
“watumishi walifundishwa namna ya kuandaa chumba cha upasuaji, kuandaa na kukagua vifaa vitakavyotumika kwenye upasuaji, pamoja na mashine ya ganzi na usingizi salama, pia namna ya kuhakiki mgonjwa kabla ya kuanza upasuaji,” amesema Dkt. Novacatus.
Watumishi walionufaika na mafunzo hayo ni watumishi wanaotoa huduma katika chumba cha upasuaji, wauguzi, na madaktari wa hospitali hiyo.
Watumishi hao pia walishauriwa kuendeleza na kusimamia utaratibu sahihi wa chumba cha upasuaji ili kuongeza ufanisi katika huduma za upasuaji na kupunguza rufaa zisizo za lazima.