Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA KUPUNGUZA RUFAA MKOANI PWANI

Posted on: June 11th, 2025

Na WAF, PWANI 


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirye Ukio amesema ujio wa timu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan katika  mkoa  wa Pwani ni hatua muhimu ya kuboresha huduma za afya na kupunguza idadi ya rufaa zinazotumwa nje ya mkoa huo.


Dkt. Ukio ameeleza hayo leo Juni 09, 2025  wakati wa ukaribisho wa Madaktari  Bingwa 64  wa Mama Samia watakaoweka kambi  ya siku sita (6)mkoani humo.



“Kwa muda mrefu tumekuwa tukilazimika kuwapeleka wagonjwa Dar es Salaam kwa ajili ya huduma za kibingwa, hivyo  Ujio wa madaktari hawa utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza rufaa na kuleta unafuu kwa wagonjwa na familia zao,” ameeleza Dkt. Ukio.


Ameeleza kuwa pango huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya awamu ya sita  chini  uongozi imara wa Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwenye ngazi ya msingi  chini ili kila Mtanzania apate huduma stahiki bila vikwazo vya kijiografia au kiuchumi.


Pia amewataka madaktari hao kuweka mipango ambayo itazidi kuboresha  huduma za  afya hasa katika maeneo ambayo yana changamoto.


"Natamani maeneo yenye usumbufu tusaidiane kuyaboresha na wale tutakaowakuta  tuwakumbushe wajibu wao kuna maeneo changamoto zinajirudia rudia  natamani mwendelee kurekebisha haya machache," amesema Mganga huyo.




Amewaomba kutoa mrejesho kwa kila ambacho watakikuta katika maeneo hayo lengo likiwa ni kuhakikisha Mtanzania anapata huduma bora za afya.


Kwa upande wake  Mratibu wa Kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia  kutoka Wizara ya Afya , Bw. Joachim Masunga amesema madakatari  bingwa na bobezi 64 wa Mama Samia  wametia timu  mkoani Pwani kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa na bobezi mkoani humo.


Wakiwa mkoani humo, watawafikia wagonjwa wenye changamoto mbalimbali, watatoa mafunzo kwa wataalam wa kada ya afya mkoani humo na wataelekeza matumizi ya vifaa mbalimbali ambavyo vimenunuliwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.


Bw.Masunga amesema lengo kubwa la ujio huo ni kwenda kutoa huduma na kuwawezesha wataalam wa afya waliopo katika vituo ili kupunguza rufaa zilizokuwa zikitokea kwenye vituo  vya kutolea  huduma kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tumbi na Hospitali ya Taifa Muhimbili.



Amefafanua kuwa kuna vifaa vingi ambavyo  vimenunuliwa na Serikali na vimepelekwa katika vituo na baadhi havijafungwa au vimefungwa lakini wale wataalam hawana zile mbinu za kiufundi.


"Ujio wenu mtaenda Kusaidia na nendeni mkafunge na muelekeze namna ya kutumia ambavyo vipo kule kwenye vituo pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wetu  ili kutoa huduma kulingana na miongozo ya Serikali,tuna imani mambo yote yanayofanyika kule yatakuwa mazuri," amesema  Bw. Masunga 


Pia Bw. Masunga ameongeza kuwa madaktari hao wanatakiwa  kuwajengea  uwezo kwenye eneo la utawala ili waweze kujiendesha vizuri na kufikia malengo ambayo yamewekwa na Serikali.