MAAZIMIO MKUTANO HUDUMA ZA CHANJO YATEKELEZWE KWA VITENDO, KUIMARISHA AFYA YA WATOTO NCHINI
Posted on: June 6th, 2026Na Mvuda Jaffer,WAF-Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Afya,Bw. Issa Ng’imba, amezitaka Mikoa na Halmashauri nchini kuhakikisha maazimio na mapendekezo yaliyotolewa katika Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Huduma za Chanjo nchini yanatekelezwa kikamilifu ili kuendelea kuimarisha afya ya watoto na jamii kwa ujumla.
Amezungumza hayo leo Juni 6,2026 wakati wa kufunga mkutano huo, Bw. Ng’imba amesema mafanikio ya programu za chanjo yanategemea usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa maazimio yaliyokubaliwa na wadau mbalimbali wa afya, huku akizitaka Mikoa na Wilaya kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maamuzi hayo.
“Ni muhimu kuhakikisha maazimio yote yaliyotolewa katika kikao hiki yanatekelezwa kwa vitendo. Hii itasaidia kuimarisha huduma za chanjo, kuongeza ufanisi wa mifumo yetu ya afya na kulinda afya ya watoto pamoja na jamii kwa ujumla,” amesema Bw. Ng’imba.
Katika hotuba yake, Bw. Ng’imba amesistiza umuhimu wa Mikoa na Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa majokofu ya kuhifadhia chanjo ili kuhakikisha upatikanaji wa vifaa hivyo katika vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha, amewaataka Waratibu wa Chanjo wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha vifaa vyote vya mnyororo baridi vinasajiliwa katika mfumo wa MEIMIS kwa mujibu wa maamuzi ya mkutano huo.
Pia ,Bw.Ng’imba ameelekeza Mikoa na Halmashauri kutenga rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kupitia mifumo ya ufuatiliaji wa ngazi ya jamii, hatua ambayo itasaidia kugundua mapema wahisiwa wa magonjwa na kuwezesha uchukuaji wa hatua stahiki kwa wakati. Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kusafirisha sampuli za uchunguzi kwa kutumia huduma za Posta ili kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa.
Bw. Ng’imba amekumbusha kuwa huduma za chanjo zinapaswa kuendelea kutolewa kila siku katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya pamoja na kupitia huduma za mkoba na tembezi ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa haki yake ya kupata chanjo kutokana na changamoto za upatikanaji wa huduma.