MAARIFA ENDELEVU NGUZO MUHIMU YA KUIMARISHA MWITIKIO WA DHARURA ZA KIAFYA
Posted on: May 31st, 2026Na Andrea Kadege, WAF-Simiyu
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yudas Ndungile, amewahimiza wataalamu wa afya waliopata mafunzo ya mwitikio wa haraka (RRT) kuendelea kujiongezea maarifa na ujuzi wa kitaalamu kwa kusoma miongozo, tafiti na nyaraka mbalimbali, akieleza kuwa maarifa endelevu ni nguzo muhimu katika kuimarisha utayari na mwitikio wa dharura za kiafya.
Dkt. Ndungile amebainisha hayo leo Mei 31, 2026 wakati akifunga mafunzo ya Timu za Mwitiko wa Haraka (RRT) yaliyofanyika mkoani Simiyu, yaliayoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Idara ya Dharura na Maafa, Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa kushirikiana Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI.
Aidha, Dkt. Ndungile amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta mbalimbali pamoja na ushirikishwaji wa jamii katika kuzuia, kugundua na kukabiliana na dharura za kiafya, akibainisha kuwa jamii ni sehemu muhimu ya mifumo ya utayari na mwitikio wa dharura.
Amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kujenga wataalamu wenye uwezo wa kufanya tathmini za haraka, kuratibu mwitikio na kutoa ushauri wa kitaalamu wakati wa matukio ya dharura za kiafya na milipuko ya magonjwa.
Kwa upande wake Mratibu kutoka Idara ya Dharura na Maafa Dkt. Simon Chacha ameeleza kuwa kuimarika kwa timu za mwitiko wa haraka kutasaidia kuongeza utayari wa mkoa katika kukabiliana dharura za kiafya na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo pamoja na vitisho vingine vya afya ya umma vinavyoweza kujitokeza wakati wowote.
Katika hatua nyingine amewapongeza washiriki kwa ushiriki wao mkubwa na kujituma katika mafunzo hayo, akibainisha kuwa maarifa na ujuzi walioupata vinapaswa kutumika kuboresha huduma za afya na kuimarisha mifumo ya mwitikio wa dharura katika ngazi zote.