Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

LISHE NI AJENDA YA RAIS SAMIA NA BADO NI KIPAUMBELE KATIKA SEKTA YA AFYA

Posted on: January 11th, 2024

Na. WAF - Dar es Salaam


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Suala la Lishe ni jambo kubwa ambalo limepewa kipaumbele katika Sekta ya Afya kwa kuwa ni ajenda kubwa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Waziri Ummy Mwalimu amesema hayo leo Januari 11, 2023 alipokutana na watumishi wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) baada ya kutolewa tamko la kufutwa kwa Taasisi hiyo na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.


“Ajenda hii ya lishe ni ajenda muhimu sana kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hii ni ajenda yake ambayo anaipa kipaumbele cha juu na sisi kama Wizara ni kipaumbele chetu.” Amesema Waziri Ummy


Aidha, Waziri Ummy amesema hakuna mtumishi yoyote wa Taasisi hiyo atakae poteza haki zake na stahiki zake za msingi ikiwemo kazi na stahiki nyinginezo.


“Kazi kubwa tunayoifanya sasa ni kujadiliana namna bora zaidi ya kuendelea kusimamia masuala ya Lishe ndani ya Wizara na pia ndani ya Serikali kwa ujumla. Waziri Ummy ameeleza kuwa kwa sasa jina la TFNC litaendelea kutumika hadi itakavyoelekezwa vinginenyo, kinachobadilika hapo ni hali ya kisheria ‘legal status’.”


Mwisho, Waziri Ummy amesema kuwa kazi na majukumu ya Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) yataendelea kama kawaida kwa kutumia bajeti yao ya mwaka wa fedha 2023/2024.


Waziri Ummy ameambatana na timu kutoka Wizara ya Afya akiwemo Katibu Mkuu Dkt. John Jingu, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu.