Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KWA MATUMIZI SAHIHI YA LISHE TUMIENI MWONGOZO WA TAIFA WA CHAKULA NA ULAJI

Posted on: November 16th, 2023


Na. WAF - Dar es Salaam


Maafisa lishe, Wataalam wa Afya, Wataalam wanaotoa Elimu ya Lishe pamoja na Watafiti watakiwa kutumia Mwongozo wa Taifa wa Chakula na Ulaji kwa kutoa elimu ya masuala ya lishe kulingana na mwongozo unavyowataka.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Novemba 16, 2023 wakati akizindua Mwongozo huo wa Taifa wa Chakula na Ulaji, uliandaliwa ili kuhamasisha matumizi sahihi ya Chakula mchanganyiko katika kutokomeza changamoto zote za Utapiamlo uliofanyika katika Soko la Kisutu Jijjni Dar es Salaam. 


“Mwongozo huu unaweza kutumiwa na kila Mtanzania na umehakisi mazingira yaliyopo nchini, na unaenda kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 12 Barani Afrika kuwa na Mwongozo wake wa Chakula na Ulaji.” Amesema Waziri Ummy


Amesema, Watanzania wanahitaji sana Mwongozo huu kwa sababu bado kuna tatizo la lishe duni nchini na tatizo hilo limekuwa kisababishi kikubwa cha utapiamlo wa aina zote katika jamii na kuchangia kushindwa kufikia kwa malengo ya kiafya na kimaendeleo kwa mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla.


“Nimeupitia Mwongozo huu nataka niwahakikishie Watanzania Mwongozo huu unaweza kutumiwa na kila Mtanzania, awe mjini, awe kijijini, awe tajiri, awe maskini, ni mwongozo ambao unahakisi mazingira ya Kitanzania.” Amesema Waziri Ummy


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema kiu kubwa ya Watanzania ilikuwa ni kufahamu ale chakula gani na chenye mchanganyiko upi na kwa kiasi gani, hivyo ujio wa Mwongozo wa Chakula na Ulaji unaenda kukidhi mahitaji hayo.


“Matumizi sahihi ya Mwongozo huu yanaenda kuleta tumaini la kuondokana na matatizo ya udumavu na kwenda kupunguza changamoto zinazoleta matatizo ya upungufu wa Madini na Vitamini kwa Watanzania.” Amesema Dkt. Germana


Mwongozo wa taifa wa Chakula na Ulaji umeandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ukiwa na malengo mahususi ya kuongeza matumizi sahihi ya chakula mchanganyika katika kaya, kuhamasisha kupunguza matumizi ya Chumvi, Sukari na Mafuta, Kuhamasisha usafi wa Mazingira yanayotumika kuandaa Chakula na kuboresha Afya na lishe za jamii.