Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KUWAIT IMEKUA MSAADA KWA TANZANIA KATIKA SEKTA YA AFYA

Posted on: February 21st, 2024


Na. WAF - Dar Es Salaam

Serikali ya Kuwait imekuwa msaada kwa Serikali ya Tanzania katika Sekta ya Afya ambapo imeweza kusaidia mipango kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa mashine za ganzi kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Uwalimu amesema hayo usiku wa jana Februari 21, 2024 Jijini Dar Es Salaam kwenye Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru na miaka 33 ya Siku ya Ukombozi wa Kuwait ambapo kwa Tanzania Maadhimisho hayo yameongozwa na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Mubarak Mohammad Alsehaijan.

“Kwa nafasi yangu kama Waziri wa Afya, kwa namna ya pekee kabisa, napenda kuishukuru Serikali ya Kuwait kwa msaada wake katika Sekta ya Afya, pamoja na kutoa msaada wa mashine za ganzi, wameweza kusaidia vifaa vya upasuaji kwa watoto wanaosumbuliwa na vichwa vikubwa (Hydrocephalus) kwenda Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).” Amesema Waziri Ummy

Amesema, Kuwait imesaidia pia kwa kutoa Vifaa Tiba katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar, Mashine za Watoto Wachanga zisizo na hewa kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Handeni, Tanga unaofadhiliwa na Taasisi ya Abdullah Al Nouri ya Kuwait.

Aidha, kwa mwaka 2023 Kuwait kupitia Kuwait Children Heart Association ilileta madaktari bingwa walioshirikiana na watalaam wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma na kufanya upasuaji wa moyo bure kwa watoto 100 wa kipato cha chini nchini.

“Hatua hizi zinaashiria kwamba uhusiano wa kindugu na urafiki uliopo kati ya nchi zetu mbili (Tanzania na Kuwait), nina imani kuwa uhusiano huu utaendelea kuwa wa karibu na chini ya uongozi wa busara, mahiri na mwanga wa viongozi wetu wawili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Sheikh Mishal al-Ahmad al. -Sabah, Amir wa Kuwait.” Amesema Waziri Ummy