KUKINGA NA KUDHIBITI MAAMBUKIZI, NGUZO MUHIMU KATIKA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: April 20th, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Morogoro
Kukinga na udhibiti wa maambukizi ni nguzo muhimu katika kuboresha ubora wa huduma za afya, kwani huchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi yanayoweza kujitokeza nchini.
Akizungumza hayo Aprili 14,2026 Mkoani Morogoro,mratibu kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Joseph Okororo katika kikao kazi cha kufanya uchambuzi wa takwimu za kukinga na kudhibiti maambukizi pamoja na kuongeza baadhi ya viashiria katika mfumo wa DHIS2,
Dkt. Okororo amesema Katika utekelezaji wa mpango huu, kuna maeneo matatu makuu yanayozingatiwa. Kwanza, ni kuhakikisha tunapambana na magonjwa yote ya kuambukiza katika hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya, jambo ambalo ni sehemu ya kuimarisha mfumo wa afya ili uwe imara na wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Ameongeza kuwa, Serikali ya awamu ya Sita inaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa yote ya kuambukiza katika hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya, hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa afya ili uwe imara na wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.
“Serikali imeendelea kudhibiti kuenea kwa vimelea vyenye usugu dhidi ya dawa (antimicrobial resistance), kwa kuhakikisha usugu huo hauenei zaidi, ili kulinda ufanisi wa tiba zilizopo na kupunguza hatari kwa jamii,” amesema Dkt.Okororo
Aidha, ameongeza kuwa uimarishaji wa maandalizi na uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa wakati ni muhimu, kupitia mifumo thabiti ya ufuatiliaji na hatua za haraka za kudhibiti maambukizi pale yanapotokea.