KONGANI YA VIWANDA VYA DAWA KUCHOCHEA MAPINDUZI YA SEKTA YA AFYA
Posted on: May 8th, 2026Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba barani Afrika kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya afya na teknolojia za kisasa. Hatua hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje ya nchi na kuongeza uwezo wa ndani wa uzalishaji wa dawa, chanjo pamoja na vifaa tiba.
Waziri Mchengerwa ameyabainisha hayo leo tarehe 8 Mei, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uendelezaji wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba, Dar es Salaam.
Waziri Mchengerwa amesema maendeleo ya kongani hiyo yatafungua fursa kubwa za ajira kwa vijana, kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kuimarisha usalama wa afya nchini.
Ameeleza kuwa Serikali imeamua kuwekeza katika sekta ya afya si kwa ajili ya huduma pekee, bali pia kama nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa taifa.
Aidha, amesema mfumo wa kongani utasaidia kupunguza gharama za uwekezaji kwa kuweka pamoja miundombinu muhimu kama maabara, mifumo ya maji, umeme na huduma za udhibiti wa ubora wa bidhaa za afya. Hatua hiyo itawavutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwa urahisi zaidi.
Waziri Mchengerwa pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu ya juu katika kujenga wataalamu wenye uwezo wa kuendesha viwanda vya kisasa vya dawa na teknolojia za afya nchini.
Ameongeza kuwa Tanzania inaendelea kujijengea mazingira bora ya uwekezaji yenye lengo la kuhakikisha bidhaa za afya zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vya kimataifa na kuweza kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.