Wizara Ya Afya

JENGENI MAZOEA YA KUCHANGIA DAMU ILI KUOKOA MAISHA

Posted on: May 31st, 2026

Na WAF, Dar es Salàam

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema wananchi wanapaswa kujenga mazoea ya kuchangia damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya maelfu ya watu wanaohitaji huduma hiyo nchini.

Waziri Mchengerwa amesema hayo leo tarehe 30 Mei, 2026 wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa damu salama nchini na juhudi zinazofanywa na Serikali kuongeza makusanyo ya damu.

Amesema Tanzania ilikusanya chupa za damu salama 512,000 mwaka 2025, hatua inayodhihirisha mwitikio mzuri wa wananchi katika kampeni mbalimbali za uchangiaji damu.

Amefafanua kuwa damu hiyo imechangia kuimarika kwa huduma za upasuaji, matibabu ya wahanga wa ajali za barabarani, huduma za uzazi salama pamoja na matibabu ya wagonjwa wa selimundu na saratani za damu.

“Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji na uhifadhi wa damu, kuongeza kampeni za uhamasishaji na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa damu salama,” amesema Mhe. Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa amewataka wananchi kuondoa hofu na dhana potofu kuhusu uchangiaji damu, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya zoezi hilo kuwa sehemu ya utamaduni wa jamii ili kuhakikisha upatikanaji wa damu salama unaendelea kuimarika nchini.