JAMII YAHIMIZWA KUACHA UNYANYAPAA KWA WATU WANAOISHI NA KIFAFA
Posted on: February 9th, 2026Na WAF-Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi (Mb), ametoa wito kwa Watanzania kuacha unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na ugonjwa wa kifafa na kuchukua hatua madhubuti za kuboresha upatikanaji wa huduma bora za matibabu kuanzia ngazi ya msingi.
Dkt. Samizi ametoa wito huo leo Februari 9, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Kifafa Duniani pamoja na Mkutano wa Kifafa Nchini ulioandaliwa na Chama cha Kifafa Tanzania (TEA), uliofanyika katika Ukumbi wa Ummy Mwalimu, Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, Naibu Waziri amesema ugonjwa wa kifafa bado umezungukwa na imani potofu katika jamii nyingi, hali inayosababisha wagonjwa wengi kuchelewa kupata matibabu sahihi na kukumbana na changamoto za kijamii, kisaikolojia na kiuchumi.
“Katika baadhi ya jamii, kifafa huaminika kuwa ni ugonjwa unaoambukiza au unaosababishwa na uchawi, jambo linalopelekea wagonjwa kunyanyapaliwa katika elimu, ajira, ndoa na hata katika maisha ya kila siku. Hali hii haikubaliki,” amesema Dkt. Samizi.
Ameeleza kuwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa takribani watu milioni 50 duniani wanaishi na kifafa, huku zaidi ya asilimia 80 ya mzigo wa ugonjwa huo ukiwa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, hususan barani Afrika. Ameongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazobeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huo, ikiwa zaidi ya watu milioni moja wanakadiriwa kuishi na kifafa, huku takribani laki mbili pekee wakipata huduma katika vituo vya afya.
Naibu Waziri amesema Serikali, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza katika Sekta ya Afya kwa lengo la kuboresha huduma za magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kifafa. Amesema upatikanaji wa dawa za kifafa umeimarika kwa kiasi kikubwa, ambapo dawa kama Carbamazepine zimefikia zaidi ya asilimia 50 na Phenobarbitone zaidi ya asilimia 90 katika vituo vya huduma za afya.
Ameongeza kuwa Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na WHO, Chama cha Kifafa Tanzania (TEA) na Taasisi ya AMREF, inaendel