IRINGA YAENDELEA KUIMARISHA UTAYARI WA KUKABILIANA NA DHARURA ZA AFYA KWA VITENDO
Posted on: October 5th, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Iringa
Iringa imeendelea kupima utayari wa kukabiliana na dharura za afya kwa vitendo, kupitia mafunzo ya timu za mwitikio wa haraka (RRT) yanayolenga kuhakikisha wataalamu wanakuwa tayari kutumia maarifa, mifumo na rasilimali zilizopo kutoa mwitikio wakati wa magonjwa ya mlipuko na matukio mengine ya afya.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 05, 2026 Mkoani Iringa na Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Sylvia Mamkwe, wakati wa mafunzo ya timu za mwitikio wa haraka yanayofanyika mkoani humo, ambapo amesema mafunzo hayo yanatoa fursa ya kupima kwa vitendo namna wataalamu walivyojiandaa kukabiliana na mazingira ya dharura yanapojitokeza.
Dkt. Mamkwe amesema sehemu muhimu ya mafunzo hayo ni zoezi la kuigiza tukio la dharura (Simulation), ambalo linawaweka washiriki katika mazingira yanayoakisi tukio halisi na kuwawezesha kutumia maarifa na ujuzi wao katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mwitikio.
Amesema kupitia zoezi hilo, wataalamu wanaweza kubaini maeneo yenye nguvu pamoja na maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya kukutana na tukio halisi, hivyo kutoa nafasi ya kufanya marekebisho yatakayoongeza utayari na ufanisi wa mwitikio wa dharura za afya.
Kwa upande wake, Afisa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Boniface Makelemo, amesema mafunzo kwa vitendo yanasaidia kuweka wataalamu katika mazingira yanayofanana na tukio halisi, jambo linalowapa nafasi ya kupima namna watakavyoshirikiana na kutumia mifumo iliyopo wakati wa kukabiliana na dharura za afya.
Dkt. Makelemo amesema zoezi la Simulation linasaidia kubaini maeneo yanayohitaji kuendelea kuimarishwa katika mwitikio, hivyo kutoa nafasi ya kufanya maboresho mapema na kuhakikisha timu zinakuwa katika utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na dharura nyingine za afya ya jami