Wizara Ya Afya

HUDUMA ZA KIBINGWA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA ZAPUNGUZA RUFAA NJE YA NCHI

Posted on: June 9th, 2026

Na Shaban Juma, Dodoma

Hospitali ya Benjamin Mkapa imeendelea kuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kutoa huduma za kibingwa na bingwa bobezi, hali inayorahisisha upatikanaji wa matibabu ya magonjwa mbalimbali ambayo awali baadhi ya wagonjwa walilazimika kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Hayo yamejiri leo Juni 09, 2026 kufuatia ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambapo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Johannes Lukumay, ameipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika hospitali hiyo.

Dkt. Lukumay amesema Hospitali ya Benjamin Mkapa inapaswa kuwa mfano kwa hospitali nyingine nchini katika utoaji wa huduma za afya pamoja na huduma kwa wateja, akieleza kuwa maoni mengi kutoka kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini hapo ni chanya.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya pamoja na wataalamu wa kada mbalimbali ili kutekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Aidha, Dkt. Samizi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kutambua namba zao za afya ikiwemo shinikizo la damu, sukari mwilini pamoja na uzito, ili kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na magonjwa hayo.