Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA TEMEKE YAZINDUA WODI YA KUSAFISHA DAMU NA GARI LA DHARURA KWA MAMA NA MTOTO

Posted on: August 12th, 2024



Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke(TRRH) imezindua rasmi jengo la Huduma za Usafishaji Damu kwa wagonjwa wa figo, pamoja na gari la dharura maalumu kwa ajili ya mama na mtoto.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 12 Agosti 2024, na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Sixtus Mapunda amewasilisha salamu kutoka kwa Waziri wa Afya, amesema Jengo hilo jipya la usafishaji damu ni moja ya maboresho makubwa yaliyofanyika hospitalini hapo, hatua ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma za usafishaji damu kwa wananchi wanaoishi maeneo ya karibu na Temeke hivyo kupunguza changamoto za kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

Mhe. Mapunda ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuwahimiza wananchi kufanya mazoezi na kupunguza ulaji wa vyakula visivyo na afya ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, na matatizo ya afya ya akili, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Dkt. Joseph Kimaro, ameeleza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na hospitali hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1970, na kusema Hospitali imefanikiwa kwa asilimia 98 kwenye suala la upatikanaji wa dawa muhimu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu na kuajiri watumishi 120 wa mkataba katika kada mbalimbali za afya ili kuboresha huduma, hususani huduma za kibingwa na bingwa bobezi.

Dkt. Kimaro ameendelea kwa kutoa shukrani kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kuchangia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa jengo la wodi ya usafishaji damu.

“nitoe wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi na kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya ili kuhakikisha huduma bora na salama zinatolewa kwa wananchi”. Amesema Dkt. Kimaro