Wizara Ya Afya

HOSPITALI WILAYA UVINZA YANUFAIKA MAFUNZO HUDUMA ZA DHARURA, MAHUTUTI KUPITIA USIMAMIZI SHIRIKISHI WIZARA YA AFYA

Posted on: April 24th, 2026



Hospitali ya Wilaya ya Uvinza imepokea mafunzo na usimamizi shirikishi kutoka kwa watalam wa Wizara ya Afya kuhusu utoaji wa huduma za dharura, ajali na wagonjwa mahututi, hatua inayolenga kuboresha ubora wa huduma za afya kwa wananchi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Uvinza, Dkt. Emanuelina Simoni ameishukuru Wizara ya Afya kwa kutembelea Hospitali hiyo na kufanya ukaguzi wa namna huduma zinavyotolewa kwa wagonjwa wa dharura na mahututi pamoja na kutoa maelekezo kuhusu matumizi sahihi ya jengo la Dharura na mpangilio bora wa vifaa.

Akizungumza leo Aprili 24, 2026 mkoani Kigoma, Dkt. Simoni amesema ujio huo wa wataalam umeleta mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya, hasa kwa wagonjwa wa dharura, ajali na mahututi.

Amesema, uongozi wa hospitali hiyo utahakikisha maelekezo yote yaliyotolewa yanatekelezwa kikamilifu ili kuboresha huduma kwa wananchi, na ameomba Wizara iendelee kutoa mafunzo na usimamizi shirikishi mara kwa mara ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Aidha, amepongeza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya nchini, hususan huduma za dharura na wagonjwa mahututi.

Kwa upande wake, Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Uvinza, Morati Kashwabi ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuratibu mafunzo hayo ya usimamizi shirikishi kazini, amesema yameboresha kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma bora za dharura kwa wananchi.