HATUA MPYA KUIMARISHA MTANDAO WA MAABARA TANZANIA
Posted on: March 13th, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Dar es Salaam
Wataalamu kutoka wizara za serikali, maabara za kitaifa, taasisi za udhibiti na washirika wa maendeleo wamekutana kujadili namna ya kuimarisha mtandao wa maabara na ufuatiliaji wa magonjwa nchini Tanzania, amesema Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bi. Mwaisha Mrisho.
Bi. Mrisho amesema hayo Machi 11, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kilichowakutanisha wizara za kisekta na taasisi kadhaa kwa lengo la kuimarisha uratibu wa ufuatiliaji wa magonjwa, kuimarisha ushirikiano wa maabara na kuongeza uwezo wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa nchini, Kilicho fadhiliwa na Shirika la Afya Duniani, Chini ya Mfuko wa Pandemic Fund.
Amesema ushirikiano wa sekta mbalimbali una nafasi muhimu katika kuzuia, kugundua na kukabiliana na magonjwa mapya pamoja na yale yanayojirudia. Ameongeza kuwa mtandao imara wa maabara ni nyenzo muhimu ya kuimarisha usalama wa afya ya taifa.
Aidha, washiriki wa kikao hicho wamependekeza kupanua wigo wa mtandao huo kwa kujumuisha sekta nyingine muhimu, ikiwemo Wizara ya Maji, kutokana na mchango wake na kudhibiti magonjwa yanayoenezwa kupitia maji kama vile kipindupindu.
Washiriki hao wamependekeza kujumuisha masuala ya usalama wa damu pamoja na kuongeza ushiriki wa taasisi za elimu na utafiti ili kuimarisha uwezo wa kitaalamu katika sekta ya maabara.
Bi. Mrisho amesema mtandao huo unakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo utegemezi mkubwa wa ufadhili kutoka kwa wahisani wa nje. Amesema ili kukabiliana na hali hiyo, wadau wanapaswa kuandaa bajeti maalum kwa ajili ya shughuli za mtandao huo ili kuhakikisha ushiriki unaungwa mkono na uongozi wa taasisi husika.
Katika hatua nyingine, washiriki walipata wasilisho kuhusu hali ya mikakati ya kitaifa ya matumizi ya teknolojia ya genomics katika ufuatiliaji wa magonjwa mapya ya kuambukiza na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
Bi. Mrisho ameongeza kuwa tathmini ya kitaifa imebainisha changamoto kadhaa, zikiwemo upungufu wa uwezo wa maandalizi ya sampuli, uhaba wa vifaa na vitendanishi vya maabara pamoja na ukosefu wa miongozo ya kitaifa.