Wizara Ya Afya

HAKUNA MTOTO ATAKAYEACHWA NYUMA - WAZIRI MCGENGERWA.

Posted on: April 30th, 2026

Serikali ya Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kutokubali jiografia kuwa kikwazo cha ukosefu wa huduma bora za afya kwa wananchi hususani watoto.

Hayo yamebainishwa na waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa makabidhiano ya boti za chanjo Bandari ya Nyamisati, Mkoani Pwani, Aprili 29, 2026 ambapo ameeleza falsafa ya Serikali ya ni kuhakikisha haki ya afya inawafikia wote bila kujali mahali wanapoishi.

"Katika afya ya umma, mtoto mmoja asiyefikiwa na chanjo si takwimu ndogo; ni swali kubwa kwa dhamira yetu ya haki, utu na usalama wa Taifa," amesema Mhe. Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa ameeeleza kuwa changamoto za kijiografia, kama vile maji yanayotenganisha ardhi, zimekuwa zikizuia baadhi ya watoto kupata chanjo.

Serikali imejipanga kuvuka vizuizi hivi kwa kujenga "daraja linaloelea," ambalo ni boti hizo saba zilizozinduliwa. Hii ni hatua ya makusudi ya kuhakikisha huduma za afya zinawafuata wananchi badala ya wananchi kuteseka kuzifuata.

Lengo la mkakati huu ni kupanua wigo wa kufikia walengwa wote, kuongeza uhakika wa usambazaji wa chanjo, na kuimarisha usimamizi shirikishi. Hii ndiyo msingi wa mfumo wa afya unaomjali mwananchi, ambapo serikali inachukua jukumu la kusogeza huduma karibu na walengwa, hasa wale wanaoishi maeneo magumu kufikika kama vile visiwani na mwambao.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa chanjo ni kinga muhimu inayomkinga mtoto leo ili taifa lisitibu janga kesho. Hii ni hekima ya kutenda mapema kabla ya matatizo hayajatokea. Kwa kuwafikia watoto wote, Serikali inajenga msingi imara wa afya kwa vizazi vijavyo na kuhakikisha kuwa taifa linakuwa salama dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Katika kuhitimisha, Waziri alisisitiza kuwa hakuna kisiwa kilicho mbali kiasi cha kusahaulika na hakuna mtoto aliye mdogo kiasi cha kutokupewa kipaumbele. Falsafa hii ndiyo inayoliongoza taifa katika safari ya kuboresha huduma za afya, ambapo kila hatua inayochukuliwa inalenga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata haki yake ya afya bila kujali eneo lake la makazi.