Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HAKIKISHENI BIDHAA ZINAZOZALISHWA NCHINI ZINA VIWANGO

Posted on: March 21st, 2025

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, ameziagiza taasisi za kudhibiti ubora wa bidhaa nchini kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinazozalishwa, hususan zile za sekta ya afya, zinakidhi viwango vya ubora vinavyohitajika ili kushindana katika masoko ya kimataifa.

Ametoa agizo hilo leo, Alhamisi Machi 20, 2025, baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mitambo ya kuzalisha oksijeni kwa matumizi ya hospitali.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini ni salama, bora, na zinakubalika kimataifa katika ofisi za TOL Gases, Temeke, Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema kuwa mradi huo, utakapokamilika, utazalisha lita milioni 4.1 za oksijeni ya matibabu kwa mwaka kuanzia 2026. "Hatua hii itaboresha upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na vituo vya afya pamoja na kupunguza gharama za oksijeni ya matibabu kwa asilimia 35 katika hospitali na vituo vya afya kote nchini, hivyo kuimarisha huduma za afya kwa wananchi," amesema Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa oksijeni ya matibabu kwa urahisi katika kila kituo cha huduma za afya nchini. "Mradi huu utaongeza upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na zahanati, kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya kupumua na kuokoa maisha ya akina mama na watoto," amesema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa mradi huu ni muhimu kwa sababu oksijeni inayozalishwa kwa njia hii inakuwa na viwango vya ubora, hivyo itasaidia kuimarisha huduma za afya na kupunguza vifo. Pia amepongeza juhudi za washirika wa maendeleo kama UNITAID, CHAI, JAPANI, CANADA, na TOL Gases kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha miundombinu ya oksijeni nchini.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases, Bw. Daniel Warungu, alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujidhatiti katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.