Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HADUBINI 133 ZAKABIDHIWA KWA AJILI YA VYUO VYA AFYA VYA KATI NA VITUO VYA TAFITI ZA MAGONJWA YA BINADAMU

Posted on: November 14th, 2023


Na. Waf - Dar es Salaam

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Mandeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI), imekabidhi Hadubini 133 na vitendanishi vingine vya maabara vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi za kitanzania Bilioni 1.2 kwa ajili ya kutumika kufundishia katika vyuo vya Wizara ya Afya vinavyo toa kozi za maabara katika Mikoa sita ambayo ni Mbeya, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Mara, na Singida.

Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika Novemba 14, 2023 katika chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUCOHAS) Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Mkuu wa Program kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali.

Dkt. Catherine amesema Hadubini hizo zitasaidia kukuza uwezo wa wataalamu wa maabara kwa kuweza kutambua kwa usahihi vimelea vya malaria kwa kuthibitisha uwepo wa vimelea hivyo ili kuwezesha wagonjwa kuanza matibabu sahihi na kwa wakati.

"Hadubini hizi na vitendanishi vingine vya maabara vilivyotolewa leo vitawezesha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kuimarisha uwezo wa kimaabara katika chunguzi na kusaidia utoaji matibabu ipasavyo, itakayopelekea kuokoa maisha ya watu na kuzuia madhara ya malaria". Amesema Dkt Catherine

Nae Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria Dkt. Samwel Lazaro ameishukuru Serikali ya marekani kwa kupata hadubini kwenda kwenye vyuo vya afya kwani ndio asilimia kubwa wana ajiriwa kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ofisi ya Afya kutoka USAID Tanzania Bi. Anne Murphy ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Afya kwa juhudi zake zilizopelekea kupungua kwa kasi kiwango cha malaria nchini Tanzania kutoka zaidi ya asilimia 14 ya watu mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8 tu mwaka 2022.