DKT. SAMIA KINARA SEKTA YA AFYA: BAJETI YAONGEZEKA, HUDUMA ZA KIBINGWA NA BINGWA BOBEZI ZASOGEZWA NDANI YA NCHI
Posted on: April 20th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dodoma
Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza bajeti ya Wizara ya Afya kwa asilimia 71, kutoka shilingi trilioni 1.03 mwaka 2021/22 hadi trilioni 1.76 mwaka 2025/26, hatua iliyoboresha huduma za afya na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amebainisha hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Amesema bajeti ya dawa imeongezeka kutoka shilingi bilioni 200 hadi bilioni 398.2, hali iliyoimarisha upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Katika juhudi za kupunguza vifo vya mama na mtoto, amesema Serikali imeongeza vyumba vya upasuaji wa dharura kwa wajawazito kutoka 390 hadi 580 nchi nzima, sambamba na kuimarisha huduma za rufaa na usafiri wa dharura kupitia mpango wa m-Mama.
Ameongeza kuwa takribani kaya laki 276 zisizo na uwezo zinatarajiwa kunufaika na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma za afya bila vikwazo vya kifedha.
Akizungumzia huduma za kibingwa, Dkt. Samizi amesema Serikali imefanikiwa kusogeza huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ndani ya nchi, ikiwemo upandikizaji wa figo katika hospitali za Benjamin Mkapa na Muhimbili, pamoja na huduma nyingine maalum zilizokuwa zikitolewa nje ya nchi hapo awali.
Amesisitiza kuwa hatua hizo zinaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri barani Afrika katika kuboresha sekta ya afya, hususan katika kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuimarisha huduma za kibingwa kwa wananchi.