Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. MOLLEL AZINDUA MFUMO WA AFYA JUMUISHI WA KIDIGITALI

Posted on: December 11th, 2024

Na, WAF-Kibaha, Pwani

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amezindua rasmi matumizi ya mfumo wa teknolojia inayotumika kuboresha utoaji wa huduma za afya (Afya-Tek) ndani ya Mfumo Jumuishi wa Kidigitali wa Afya ngazi ya jamii.

Hafla hiyo ilifanyika leo Desemba 10, 2024 Kibaha mkoani Pwani na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon John, wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wakiwemo wataalam wa teknolojia, wawakilishi wa mashirika ya maendeleo na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Aidha, Dkt. Mollel amesisitiza umuhimu wa mfumo huu wa kidigitali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi akibainisha kuwa mfumo wa Afya- Tek utaimarisha uratibu wa huduma za afya ngazi ya jamii, kuongeza uwazi, na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakati.

“Mfumo huu unaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya. Unatupa uwezo wa kufuatilia, kupanga, na kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote, hususan wale wa vijijini. Ni hatua muhimu katika kufanikisha azma yetu ya kuwa na afya kwenye kiganja cha mkono kupitia teknolojia,” amesema Dkt. Mollel.

Pia, amesema kuwa, Mfumo wa Afya-Tek umeunganishwa na mifumo mingine ya kidigitali nchini, hatua inayotekeleza agizo la Rais la kuhakikisha mifumo yote ya kidigitali inasomana kwa ufanisi. Hadi sasa, asilimia 80 ya mifumo hiyo imeunganishwa, na Serikali inalenga kufikia asilimia 100 katika kipindi kifupi kijacho.

Dkt. Mollel pia amewataka wadau wa maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi hizi kwa kutoa rasilimali na msaada wa kifedha ili kuhakikisha mfumo huu unafikia maeneo yote ya nchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Ndg. Nickson John amesema kuwa, wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika mkoa wa Pwani wamekua msaada mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma bora za afya katika ngazi ya chini kabisa jambo ambalo limewapa ushindi katika wilaya ya Kibaha.

Uzinduzi wa mfumo huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuboresha sekta ya afya kupitia matumizi ya teknolojia, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuimarisha huduma kwa wananchi na kuhakikisha maendeleo endelevu katika sekta ya afya.