Wizara Ya Afya

DKT. MAGEMBE AKAGUA HATUA ZA UDHIBITI WA MAGONJWA MIPAKANI - KAGERA

Posted on: May 31st, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Kagera

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema bandari ya Kemondo iliyopo mkoani Kagera ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayopokea idadi kubwa ya wasafiri kati ya 700 hadi 800 wengi wakiwa wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi, jambo linalohitaji kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji na uchunguzi wa afya ili kuzuia kuingia kwa magonjwa ya mlipuko nchini.

Dkt. Magembe amesema hayo leo Mei 31, 2026 akiwa katika ziara ya kutembelea maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kutoa huduma za dharura, vituo vya afya pamoja na maeneo ya mipakani mkoani Kagera kwa lengo la kukagua maandalizi ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko endapo atatokea mgonjwa wa Ebola.

"Bandari hii ya Kemondo ni kitovu kikubwa cha biashara, hususan biashara ya samaki na dagaa, na hupokea mamia ya watu kila siku wanaoingia na kutoka kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo kutoka nchi ya Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na wasafiri kutoka Mkoa wa Kigoma, hivyo ni lazima tuimarishe uchunguzi wa afya kwa kila anaeingia na kutoka” amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema Serikali imeendelea kuimarisha maeneo ya uchunguzi wa afya ili kurahisisha upimaji na ukusanyaji wa taarifa muhimu za wasafiri kwa wakati pamoja na kuhakikisha mifumo ya uchunguzi na ufuatiliaji inafanya kazi kwa ufanisi kutokana na wingi wa wasafiri wanaopita katika maeneo ya mipakani. Hatua hii inalenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa haraka na kuchukua hatua stahiki endapo kuna muhisiwa au mgonjwa.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kuvuka mipaka kutokana na ongezeko la wasafiri na biashara kati ya Tanzania na nchi jirani.