DKT. MAGEMBE AHIMIZA WATUMISHI WA WIZARA YA AFYA KUFANYA MAZOEZI KULINDA AFYA ZAO
Posted on: July 6th, 2026Na Happyness Hans, WAF – Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amewahimiza watumishi wa Wizara hiyo kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya mwili kwa kuzingatia ratiba maalumu iliyoandaliwa na Wizara, ili kuimarisha afya zao, kuongeza ufanisi kazini na kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Dkt. Magembe ameyasema hayo leo, Julai 6, 2026, katika Ofisi za Wizara ya Afya zilizopo Mtumba, jijini Dodoma, wakati wa hafla fupi ya kumpokea rasmi akiwa Katibu wa wizara hiyo baada yakuteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wq Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema uongozi wa Wizara utaendelea kuhamasisha ushiriki wa watumishi katika programu za mazoezi, akibainisha kuwa yeye mwenyewe atakuwa mstari wa mbele kushiriki katika kufanikisha adhma hiyo.
"Watumishi wote tusisahau kufanya mazoezi, hata mimi nitakuwa mstari wa mbele kushiriki kwenye siku zetu za mazoezi hivyo nawahimiza kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kulinda afya zetu," amesema Dkt. Magembe.
Amefafanua kuwa kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kuimarisha afya ya mwili na akili na kinga, kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza uwezo wa watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, amewataka watumishi kuzingatia ratiba ya mazoezi iliyowekwa na Wizara na kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo, akisisitiza kuwa afya bora ni msingi wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.